Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kigali
Mkutano wa Kimataifa unaofanyika jijini hapa kuzungumzia haki mazingira umeingia siku ya tatu ambapo Majaji na Mahakimu kutoka Jumuiya ya Madola wameendelea kujadili mada mbalimbali.
Mapema leo tarehe 10 Septemba, 2024 washiriki wa Mkutano wamepitishwa katika mada kadhaa, ikiwemo kurejesha haki baada ya machafuko.
Mada hiyo iliwasilishwa na kujadiliwa na Majaji Hassan Abubakar Jallow kutoka Gambia aliyezungumza kwa njia ya mtandao, Jaji Bernard McCloskey kutoka Ireland ya Kaskazini na Jaji Geraldine Umugwaneza kutoka Rwanda.
Baadaye wajumbe wa Mkutano walipitishwa kwenye mada inayozungumzia “kuhakikisha Mahakama zetu zinaweza kushughulikia mashauri yanayohusu mazingira.”
Mada hiyo iliwasilishwa na kujadiliwa na Jaji Mstaafu Emmanuel Ugirashebuja kutoka Rwanda, Jaji Mkuu Sir Gibuma Gibbs Salika kutoka Papua New Guinea, Lord. Robert Carnwath kutoka England na Wales na Jaji Charles Mkandawile kutoka Malawi.
Uwasilishaji katika Mkutano huo utaendelea kesho tarehe 11 Septemba, 2024 ambapo wataalam waliobobea kwenye maeneo mbalimbali, akiwemo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi atawasilisha mada kuhusu “upokeaji wa ushahidi unaotokana na kompyuta.”
Ufunguzi rasmi wa Mkutano huo ulifanyika jana tarehe 9 Septemba, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Kagame alisema, pamoja na mambo mengine, kuwa utungaji wa sheria na sera za mazingira ni muhimu katika kujenga mustakabali safi na endelevu zaidi.
“Muhimu zaidi ni kuwa na Mahakama imara na huru inayotekeleza sheria na kutanguliza maslahi ya wananchi,” alisema.
Mhe. Kagame alidokeza kuwa duniani kote, halijoto inaongezeka kwa viwango visivyo na kifani, huku ubora wa hewa ukizidi kupungua, jambo linalomweka mwanadamu hatarini.
“Kuna mengi yanayoweza kufanywa kulinda mazingira na kutoa haki pale inapostahili kama kutakuwepo na ushirikiano wa karibu na watekelezaji wa pamoja wa sheria na Majaji huru na wazoefu,” alisema.
Aliwataka Mahakimu na Majaji kutumia jukwaa hilo kujadili changamoto ya rushwa na mlundikano wa mashauri, huku akibainisha kuwa uhalali wa mfumo wowote wa haki utatokana na imani waliyonayo wananchi ndani yake.
Kabla ya ufunguzi huo, siku ya kwanza tarehe 8 Septemba, 2024, Majaji Wakuu walikutana kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili wanapotekeleza majukumu ya utoaji haki kwenye maeneo yao.
Siku hiyo pia kulifanyika kikao cha wajumbe wa Baraza la Chama cha Mahakimu na Majaji kutoka Jumuiya ya Madola kabla ya wageni wengine kuanza kujiandikisha kwa ajili ya Mkutano huo.
Katika Mkutano huo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameongozana na Majaji wawili wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wengine wa Mahakama Kuu.
Viongozi wengine ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Katibu wa Jaji Mkuu, Katibu wa Jaji Kiongozi na Katibu wa Msajili Mkuu.
Wapo pia Viongozi wa JMAT wa ngazi mbalimbali na Mahakimu wengine. Mkutano huo wenye kauli mbiu ya “Haki Mazingira” umeandaliwa na Jumuiya ya Madola kwa kushirikiana na Mahakama ya Rwanda.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni