• Afanya ziara ya ukaguzi Uvinza, Gereza la Wilaya Kigoma
• Apongeza kazi nzuri ya uondoshaji mashauri Uvinza
Na AIDAN ROBERT, Mahakama –Kigoma
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza amesema Mahakama ya Tanzania kupitia Mfumo wa Uratibu na Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) imeweka wazi juu ya hatua mbalimbali za mashauri kwa kila Jaji na Hakimu katika kituo chake, hivyo ni wazi kuwa mashauri mlundikano hayakubaliki Mahakamani.
Mhe. Kahyoza aliyasema hayo jana tarehe 23 Septemba 2024, alipokuwa akifanya ukaguzi wa kawaida wa Mahakama ya Wilaya Uvinza na Magereza ya Wilaya Kigoma ikiwa ni katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania.
Alisema ni vyema kushughulikia changamoto kabla ya kuzalisha mashauri ya mlundikano katika Kituo na kusisitiza kuwa, Mahakama za Mwanzo mbili ya Mgambo na Kalya ambazo hazitoi huduma ziangaliwe kwa jicho la umuhimu ili wananchi wanaoishi katika maeneo hayo ambayo ni kilometa 71 kutoka ilipo Mahakama ya Wilaya Uvinza wasogezewe huduma.
“Kwa umuhimu wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ni vyema Mahakama hizi tukaona ni kwa jinsi gani Mahakama hizi za Mwanzo Mgambo na Kalya zinaweza kufanya kazi ili kuwapunguzia gharama wananchi wa maeneo hayo ambao wanakosa haki yao ya msingi ya kupata huduma za kimahakama,” alisema Jaji Kahyoza.
Aidha, alisema pamoja na uchache wa watumishi wa Mahakama ya Wilaya hiyo ambayo pia ina Hakimu mmoja pekee, ameona kazi nzuri wanayofanya na kuwapongeza kwa takwimu nzuri za kumaliza mashauri 161 kwa miezi tisa.
Pamoja na mambo mengine, Mhe. Kahyoza alisisitiza weledi, uadilifu na uchapakazi kwa watumishi hao ikiwa ni pamoja na kusoma Mkataba wa Huduma kwa Mteja wa Mahakama ili kuendelea kujikumbusha wajibu katika kutoa huduma stahiki kwa wananchi hasa wanaofika katika Ofisi za Mahakama.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya Uvinza, Mhe Misana Majula, akitoa taarifa ya utendaji kwa Jaji Kahyoza alisema kwamba, Mahakama ya Wilaya Uvinza ni moja ya Mahakama mkoani Kigoma yenye mashauri mengi yanayoskilizwa na Hakimu mmoja tu.
Mhe. Majula alisema kuwa, jumla ya mashauri 134 yamesajiliwa kutoka Januari mpaka Septemba mwaka huu na kati ya hayo 161 yameamuliwa na kubaki mashauri 66 ambayo yanaendelea kusikilizwa mahakamani hapo.
Katika ziara hiyo ya ukaguzi, Jaji Kahyoza vilevile alipata fursa ya kuambatana na Wadau wa Haki Jinai kutembelea Gereza la Wilaya ya Kigoma kwa ajili ya ukaguzi wa kawaida wa Gereza hilo ili kujionea na kutatua changamoto walizo nazo wafungwa zinazohusiana na mwenendo wa mashauri yao mahakamani.
“Mahakama na Wadau wake tutaendelea kutatua changamoto zenu kwa karibu ili haki zenu za msingi zisichelewe, ndio sababu tuna utaratibu wa kuja kutembelea Magereza ili kufahamu na kupokea changamoto hizo na kuzitatua,” alisema Mhe. Kahyoza.
Hata hivyo, Jaji huyo alisisitiza matumizi ya Mfumo wa e-CMS kwa Wadau wake ili kuwa na uelewa sawa katika kushughulikia mashauri ya wafungwa na mahabusu waliopo katika Gereza hilo la Bangwe sambamba na kuwafahamisha wadau wote juu ya Mahakama kupunguza matumizi ya karatasi na kutumia mifumo kusikiliza mashauri pamoja na kutoa nakala laini kwa wadau wa mashauri yanayoendelea mahakamani kwa ujumla wake.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Gereza hilo, Inspekta Geofrey Bitalisha aliishukuru Mahakama na Wadau wake waliofika gerezani hapo kwa ajili ya kusikiliza na kutatua changamoto za wafungwa na Mahabusu walipo katika Gereza hilo na kuongeza kuwa, maelekezo yote yaliyotolewa na Jaji Kahyoza yatafanyiwa kazi ili kwenda na kasi ya Mahakama katika kutoa haki kwa wafungwa na Mahabusu waliopo katika Gereza hilo.
Katika ziara hiyo ya ukaguzi, Mhe. Jaji Kahyoza aliambatana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Mtotay, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Kigoma, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Uvinza na kwa upande wa Wadau aliambatana na Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Ofisi ya Mashtaka Mkoa Kigoma na Afisa Uhamiaji Msaidizi wa Mkoa wa Kigoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni