Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Abdalah
Sagini leo tarehe 23 Septemba, 2024 ametembelea Ofisi za Tume ya Utumishi wa
Mahakama jijini Dar es salaam na kuzungumza na Watumishi wa Sekretariet ya Tume
hiyo.
Ziara ya Naibu Waziri huyo ni ya kwanza katika ofisi hizo
za Tume tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo hivi karibuni.
Katika ziara hiyo ya kikazi, Naibu Waziri Sagini
alipokewa na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye ndiye Mtendaji Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel ambapo pamoja na mambo mengine
alipata wasaa wa kuzungumza na Watumishi wa Sekretariet ya Tume hiyo.
Akizungumza na Watumishi wa Sekretariet ya Tume ya
Utumishi wa Mahakama, Naibu Waziri
Sagini ameipongoza Tume kwa kuendesha mchakato wa upatikanaji wa ajira za
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania kwa njia ya kielekitroniki ambapo amesema
hatua hiyo itasaidia kuongeza uwazi na kupunguza malalamiko.
“Naipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuendesha zoezi la ajira kwa
njia ya kielekitroniki, hatua hii itasaidia sana katika kuongeza uwazi na
kupunguza malalamiko na kutokuwepo kwa upendeleo”, alisisitiza Mhe. Sagini.
Naibu Waziri huyo pia aliishukuru Serikali ya awamu ya
sita kwa kuiwezesha Tume ya Utumishi wa Mahakama kutekeleza vema majukumu yake
hususan katika bajetti na upatikanaji wa nafasi za ajira ya Watumishi wa
Mahakama ya Tanzania.
Akizungumzia Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa
na Wilaya, Naibu Waziri Sagini ameshauri Kamati hizo kutenga fedha kwa ajili ya
vikao vya kamati vilivyopo kwa mujibu wa Sheria vinavyotakiwa kufanyika mara nne
kwa mwaka.
Alisema kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itasaidia katika kuitangaza
Tume ya Utumishi wa Mahakama na kutoa elimu kwa wananchi kwa njia mbalimbali ili
waweze kufanya juu ya uwepo wa kamati zinazopokea malalamiko ya wananchi
yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya Maafisa Mahakama ili wazifahamu na
kuzitumia.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel ili
kuhakikisha wananchi wanapata uelewa kuhusu utendaji kazi wa Kamati za Maadili
ya Maafisa Mahakama, Tume itaendelea kutoa elimu kwa njia mbailimbali ili
kuwafikia wananchi wengi zaidi.
“Tutaendelea kuelimisha Umma kuhusu uwepo wa Kamati
zinazopokea malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Maafisa Mahakama kwa
njia mbalimbali ikiwemo vipindi vya Redio na Televisheni” alisisitiza Katibu wa
Tume.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo
cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya
Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili
kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la
kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja
na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa
Mahakama Sura ya 237.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Abdalah Sagini akizungumza wakati alipotembelea Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dar es salaam na kuzungumza na Watumishi wa Sekretariet ya Tume leo tarehe 23 Septemba, 2024.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Abdalah Sagini akikaribishwa kwenye Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama na Katibu wa Tume hiyo ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 23 Septemba, 2024. Anayetazama ni Naibu Katibu wa Tume (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Abdalah Sagini na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel Wakijadiliana jambo.
Sehemu ya Watumishi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wakimsikiliza Naibu Waziri.Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Abdalah Sagini (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama mara baada ya kuzungumza nao alipotembelea ofisi za Tume leo jijini Dar es salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni