Na MWANDISHI WETU- Dar es Salaam
Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert ametoa wito kwa madalali na wasambaza nyaraka za Mahakama kutekeleza vema majukumu yao ili kuepuka malalamiko ya wananchi ambayo yataleta athari hasi kwa Mhimili huo, wao binafsi, familia na taifa kwa ujumla.
Mhe. Herbert ametoa wito huo wakati akifungua mafunzo ya 13 ya watu wenye nia ya kufanya kazi ya Udalali na Usambazaji wa Nyaraka za Mahakama zaidi ya 27 kutoka katika mikoa mbalimbali nchini, jana tarehe 23 Septemba, 2024 katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania), jijini Dar es Salaam.
“Endapo mtafanikiwa kuhitimu mafunzo yenu na kusajiliwa mtakuwa maafisa wa Mahakama ambao mtapewa jukumu la kutekeleza amri halali za Mahakama. Jukumu hilo msipolitekeleza vyema mtalalamikiwa kwa kutokuwatendea haki wananchi na kwa hiyo ni dhahiri kuwa Mahakama pia itakuwa imelalamikiwa,” amesema Mhe. Herbert.
Vilevile Msajili huyo amewakumbusha washiriki hao, kuwa kosa dogo linaloweza kujitokeza katika utendaji wao wa kazi halitakuwa madhara kwao peke yao bali litakuwa na madhara kwa familia zao, Mahakama na taifa kwa ujumla, hivyo wanapaswa kuzingatia kanuni, taratibu, miongozo na maadili ya kazi yao.
Hata hivyo, Mhe. Msajili amewaambia washiriki hao kuwa kila kazi ina malalamiko lakini malalamiko hayo yatakosa uhalali endapo tu kazi hiyo itatekelezwa kwa haki na uadilifu.
“Msihofu kuhusu malalamiko ili mradi mmetenda haki. Kazi ya kutoa haki siku zote inakaribisha kulalamikiwa. Lakini lalamiko lolote linalotokana na kutimiza wajibu wa haki ni baraka na lalamiko linalotokana na kupindisha haki ni laana.,” amesema Mhe. Herbert.
Mafunzo hayo yameandaliwa na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambacho kimekuwa kikendesha mafunzo haya kwa mujibu wa Kanuni ya 4 na ya 6 za Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama Na.363 za mwaka 2017.
Kwa upande wake, mratibu wa mafunzo hayo Mhadhiri kutoka IJA Bi. Fatuma Migomba amesema kuwa malengo ya mafunzo hayo ni kuwawezesha wananchi mbalimbali wenye sifa na nia ya kufanya kazi hiyo kupata ujuzi na maarifa ili waweze kufanya shughuli hizo kwa kuzingatia kanuni, taratibu, sheria, maadili, uweledi na ufanisi.
Ameongeza kuwa mtu anapopata mafunzo hayo anakuwa ameiva katika kutekeleza amri za Mahakama kwa kuwa mafunzo yanaendeshwa kivitendo zaidi na wawezeshaji ni maafisa wabobevu kutoka wa Mahakamani ambao wengine ni Majaji na Mahakimu.
Mafunzo hayo yatafanyika kwa muda wa wiki mbili hadi tarehe 07/10/2024, ambapo Washiriki watafanya mitihani ya kupima umahiri wao na watakaofaulu watapatiwa vyeti vya umahiri vinavyowapa sifa ya kuomba na kufanya kazi hiyo.
Wahitimu watakuwa na sifa za kuweza kuajiriwa na Mahakama, wengine kufanya kazi ya minada (auctions) kama vile ya Benki na Taasisi zingine za Serikali na binafsi.
Nayo baadhi ya washiriki akiwemo dalali wa Mahakama Bw. Mkasiwa M. Mkasiwa kutoka kampuni ya Udalali ya Mart and Mkasiwa Court Broker ya Kahama mkoani Shinyanga ambaye kwa sasa anasomea mafunzo ya usambazaji wa nyaraka za Mahakama, amesema kuwa mafunzo hayo yanamsaidia mshiriki kutekeleza kwa umahiri na uweledi majukumu yake.
“Mafunzo haya yanakupa uzoefu wa kufanya kazi zako vizuri, huko nyuma nilikuwa nafanya kazi zangu za udalali bila mafunzo ila baada ya kupata mafunzo hayo mwaka jana na kuhitimu, kwa sasa kazi zangu za udalali zimekuwa zikienda vizuri zaidi,” amesema Bw. Mkasiwa.
Naye Bi. Rehema Kombo kutoka mkoani Tanga amesema kuwa ameamua kujiunga na mafunzo hayo ili apate sifa za kufanya kazi za usambazaji nyaraka za Mahakama na vilevile aweze kufahamu vema jinsi ya kutekeleza amri za Mahakama kwa haki na kwa usahihi.
Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert akifungua mafunzo ya 13 ya watu wenye nia ya kufanya kazi ya Udalali na Usambazaji wa Nyaraka za Mahakama zaidi ya 27 kutoka katika mikoa mbalimbali nchini, tarehe 23 Septemba,2024 katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania), jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa mafunzo ambaye pia ni Mhadhiri kutoka IJA Bi. Fatuma Migomba akitoa neno la ukaribisho kwenye mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni