MAHAKIMU WAKAZI WATAKIWA KUTENDA HAKI ILI KUJENGA IMANI YA WANANCHI
Na YUSUF AHMADI-Lushoto, IJA
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Mteule amewasihi Mahakimu wakazi kutenda kazi zao kwa uweledi, uwazi, haki na uadilifu ili maamuzi yao mahakamani yaweze kuheshimiwa na wananchi wanaokwenda kwao kutafuta haki.
Mhe. Mteule amezungumza hayo jana tarehe 23 Septemba,2024 wakati akifungua Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya ishirini na nane (28) katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) mkoani Tanga, kwa niaba ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani.
“Ni lazima tuwe na uwazi, weledi, na uadilifu katika utendaji wetu wa kazi ili wananchi waweze kutuamini na kuheshimu maamuzi yetu. Wananchi watajenga imani na sisi na maamuzi yetu pale tu tutakapotenda haki kwa wakati na ambayo itaonekana kutendeka,” amesema Mhe. Mteule.
Vilevile Mhe. Jaji Mteule amesema kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo Mahakama inaimarisha utoaji utoaji haki na hivyo kuwasihi kutoa haki kwa wakati, kwa ufanisi na bila kujali hali ya mtu.
Aidha, Mhe. amewadokeza washiriki hao kuwa katika utendaji wao wa kazi watarajie kukosolewa na kupongezwa huku akiwakumbusha hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye aliwahi kusema kuwa kazi yao ni ya umma na hivyo hawapaswi kupiga kelele wanapokosolewa bali wawaelimishe wanaokosoa kwa kuwa wapo wanaokosoa kwa kutokuelewa jambo.
Mafunzo hayo yatakayofanyika mpaka tarehe 4 Oktoba, 2024 yameandaliwa na kuendeshwa na IJA kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania na yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi na maarifa muhimu yatakayowaongoza katika utendaji wao wa kazi. Wawezeshaji waliopo kwenye mafunzo hayo ni Majaji, Naibu Wasajili, maafisa wengine waandamizi wa Mahakama ya Tanzania pamoja na viongozi hao wa dini.
Kwa upande wake Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Nkya amewasisitiza washiriki hao kwenda kuonesha utendaji wao kwa viwango vya juu na wazingatie maadili ya kazi yao.
Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu IJA ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mkuu Mhe.Dkt. Patricia Kisinda amewataka washiriki haokwenda kufanyia kazi mafunzo hayo ili iwe nyenzo muhimu ya utoaji haki.
Nao baadhi ya washiriki akiwemo Hakimu Mkazi Mhe. Zuhura Hamza ametaja matarajio yake baada ya mafunzo hayo ni kwenda kutekeleza kazi yake kwa uadilifu, uweledi ili kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama.
“Matarajio yangu ni kutenda kazi yangu kwa uadilifu, uweledi na uwajibikaji ili kuweza kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama, tufahamu hii kazi ni ya kijamii zaidi hivyo tunapaswa kuitumikia jamii hiyo kwa haki na uadilifu mkubwa,” amesema,” Mhe. Zuhura.
Naye Hakimu Mkazi Mhe. James Kapele amesifu mafunzo hayo kwa jinsi yalivyoandaliwa na kwamba ana imani atatoka akiwa ameiva na hivyo kwenda kutekeleza vema jukumu la kimsingi la utoaji haki.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021/22-2024/25, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja na Mpango Mkakati wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wa mwaka 2024/25-2026/27.
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Chiganga Mashauri Tengwa akizungumza wakati wa mafunzo hayo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi.
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni