Jumatano, 25 Septemba 2024

WADAU WA HAKI JINAI WAKUTANA NA HAKIMU MKAZI MFAWIDHI KIGOMA

Mhe. Tarimo awaomba ushirikiano katika kutatua changamoto za usikilizwaji wa mashauri mahakamani 

Na AIDAN ROBERT, Mahakama- Kigoma

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo amepokea ugeni wa wajumbe wa haki jinai waliofika kujitambulisha kwake kwa nia ya kufahamiana na kukuza ushirikiano wa kitaasisi na katika usikilizwaji wa mashauri mahakamani. 

Akizungumza na wadau hao jana tarehe 24 Septemba, 2024, Mhe. Tarimo aliwashukuru kwa upendo na kufika ofisini kwake kwa ajili ya kujitambulisha na kufahamiana lengo likiwa ni kuimarisha mahusiano ya kitaasisi.

“Ujio wenu kwa umoja wenu ni faraja kwamba ushirikiano wenu ni mkubwa na utaisaidia Mahakama kufanya kazi yake kwa weledi mkubwa endapo kila mmoja wetu atafanya wajibu wake kwa ufanisi, kwakuwa mpango Mkakati wa Mahakama unatutaka kuwajibika kwa viwango vinavyokubalika katika kumaliza mashauri mahakamani,” alisema Mhe. Tarimo.

Aidha, amewataka kushirikiana kwa karibu katika kuisaidia Mahakama hiyo kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa wa usikilizwaji wa mashauri ambayo yapo mbele ya Mahakama hiyo.

Aliongeza kuwa, Wadau hawatakiwi kuwa chanzo cha mlundikano wa mashauri mahakamani kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika au kutatuliwa ndani ya muda na kufanya Mahakama kuendelea na usikilizwaji wa mashauri husika, hivyo amebainisha kuwa hatoruhusu changamoto ndogondogo kukwamisha umalizwaji wa mashauri mahakamani.

 Mfawidhi huyo alisema, Mahakama imejipambanua katika mifumo ambayo wadau wote wameshirikishwa kikamilifu ili kuitambua na kuitumia ili kuisaidia Mahakama kufanya kazi yake vyema.

Kwa upande wake Afisa Upepelezi Makosa ya Jinai Mkoa wa Kigoma (RCO), Bw. Alfred Kasoro alisema kwa niaba ya wadau hao kuwa watatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha Mahakama inafanya kazi yake vizuri na wadau wote watafanya wajibu wao kisheria ili kuweza kuharakisha haki za watu mahakamani. Aidha, amemkaribisha Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo wa Kigoma. 

Wadau waliofika Mahakamani hapo ni Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Kigoma, Afisa Uhamiaji Msaidizi kutoka Mkoa wa Kigoma, Afisa kutoka Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkuu wa Gereza la Wilaya Bangwe, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanasheria wa Kujitegemea (TLS) na Afisa wa huduma kwa Jamii Mkoa.

Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wadau. Kulia ni Mkuu wa Ofisi ya Taifa Mashtaka, Bw. Abel Sanga, kushoto ni Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO),  ACP.  Alfred Kasoro na waliosimama nyuma ni sehemu ya wadau wa Haki jinai Mkoa wa Kigoma. 

 

Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo akizungumza jambo na Wadau wa Haki Jinai waliofika ofisini kwake jana tarehe 24 Septemba, 2024 kwa lengo la  kufahamiana na kupanga mikakati ya utendaji kazi kwa ushirikiano na Mahakama.

Sehemu ya wadau wa haki jinai wa Mkoa wa Kigoma wakimsikiliza kwa Makini Hakimu Mkazi Mfawidhi  Mkoa Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza nao ofisini kwake.

Wadau wa haki jinai Mkoa wa kigoma wakimsikiliza Hakimu Mkazi Mfawidhi  Mkoa Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo  (aliyeketi mbele) alipokuwa akizungumza nao ofisini kwake jana tarehe 24 Septemba, 2024.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni