Jumatano, 25 Septemba 2024

MADALALI, WASAMBAZA NYARAKA WA MAHAKAMA TABORA WATAKIWA KUWAJIBIKA

Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Mwajuma Kadilu amewataka Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kuhakikisha kuwa wanawajibika katika utekelezaji wa tuzo na amri za Mahakama sambamba na kutoa elimu kuhusu shughuli zao.

Mhe. Dkt. Kadilu aliyasema hayo jana tarehe 24 Septemba, 2024 ofisini kwake Mahakama Kuu Tabora wakati akiongoza kikao cha Kamati Ndogo ya Uteuzi na Usimamizi wa Nidhamu ya Madalali wa Mahakama na Wapeleka Wito wa Mahakama. 

“Kama mnavyofahamu Madalali na Wasambaza Nyaraka ni wadau muhimu katika utekelezaji wa tuzo na amri za Mahakama hivyo ni wadau muhimu wa kimkakati lakini bado wadau na wananchi hawana elimu ya kutosha kuhusu shughuli zao hivyo ni muhimu kuhakikisha elimu kuhusu shughuli zao ni jambo la kuzingatiwa katika mipango yetu kama Kanda,” alisema Mhe. Dkt. Kadilu.

Katika kikao hicho, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Rhoda Ngimilanga alieleza kuwa Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora wanajitahidi kufanya majukumu yao kwa mujibu wa matakwa ya kisheria na Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora unajipanga kuhakikisha wadau wa Mahakama wanapata elimu kupitia majukwaa mbalimbali mbalimbali ikiwemo Vyombo vya Habari na wakati wa maandalizi ya Wiki ya Sheria.

Wakati huohuo, Dalali wa Mahakama, Bw. Albert Sitta alieleza kuwa, Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka zina changamoto ambazo zinatakiwa kufanyiwa marekebisho.

“Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka zimekuwa mwongozo mzuri katika utekelezaji wa majukumu yetu japo kuna maeneo kadhaa yanayotakiwa kufanyiwa marekebisho kwani kuna baadhi ya rejea zinakinzana na maana iliyokusudiwa katika kanuni hizo,” alisema Bw. Sitta.

Kamati Ndogo ya Uteuzi na Usimamizi wa Nidhamu ya Madalali wa Mahakama na Wapeleka Wito wa Mahakama ilianzishwa kwa lengo la kujadili nidhamu na utekelezaji wa shughuli za Madalali na Wasambaza nyaraka wa Mahakama ili kuleta tija katika majukumu yao.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Mwajuma Kadilu Juma (aliyeketi kushoto) akiongoza kikao cha Kamati Ndogo ya Uteuzi na Usimamizi wa Nidhamu ya Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kilichofanyika jana tarehe 24 Septemba, 2024 Mahakama Kuu Tabora.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Mwajuma Kadilu Juma akisikiliza kwa umakini hoja za wajumbe wakati wa kikao cha Kamati ya Maadili ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kilichofanyika jana tarehe 24 Septemba, 2024.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Mkoa wa Tabora, Wakili Kelvin Kayaga (kulia) akifafanua jambo katika kikao cha Kamati ya Maadili ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama. Kushoto ni Mwansheria wa Serikali,Wakili Tunosye Luketa.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni