Na TAWANI SALUM-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, amesema Mahakama itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, katika mambo mbalimbali yanayohusu sekta ya sheria, likikwemo suala la akili bandia.
Kauli hiyo imetolewa jana tarehe 25 Septemba, 2024 na Jaji Mkuu, wakati alipotembelewa na Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Ally Possi katika Ofisi yake iliyopo Mahakama ya Rufani Tanzania, jijini Dar es Salaam.
“Mara nyingi Wahe. Majaji huwa tunajifunza mengi kutokana na hoja na tafiti zenu mahakamani na kuna maeneo naomba tuendeleze ushirikiano wa karibu zaidi. Kuna maeneo mapya ambapo kwa sasa yanatikisa ulimwengu kwa mfano suala la akili bandia (Artificial Intelligence) duniani kote mwezi huu mwanzoni Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa kuhusu ushauri kuhusiana na faida, changamoto na hasara za akili bandia,amesema Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma.
Aidha Mhe. Jaji Mkuu ameongeza kuwa suala la akili bandia kwa sasa limeshafika na lazima litagusa shughuli za utoaji wa haki na za kimahakama hivyo ni eneo ambalo Mahakama inahitaji kushirikiana na Ofisi hiyo ili kuangalia ni “namna gani tutavuna faida za akili bandia na vilevile tuwe na tahadhari ya changamoto ambazo zinazoweza kujitokeza kwa sababu tunaambiwa faida ni nyingi, lakini vilevile kuna mambo ambayo yanahitaji tahadhari yamebadilisha sheria,”.
Alisema mambo hayo yamebadilisha ukweli na imefikia hatua hata nchi zilizoendelea kama Australia zimeanza kutunga sheria kujaribu kupambana na taarifa za kweli na zisizo za kweli kwa sababu taarifa inaweza kusambaa ukadhani ina ukweli kumbe inakuwa imetengenezwa na akili bandia.
Hivyo jambo linalotakiwa kufanyika kwa sasa ni namna gani wataweza kujitayarisha katika mfumo wa sheria, huku akiongeza kwamba ofisi hiyo ina mchango mkubwa.
Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma amempongeza Mhe. Possi pamoja na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Alice Mtulo kwa imani kubwa ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameionesha kwao, akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kusimamia sekta muhimu ya sheria.
“Vilevile nawapongeza watumishi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambao kwa kweli ndio tunafanya nao kazi kila siku kwa pamoja na ukiangalia majukumu makubwa ambayo ofisi yako imepewa inaonyesha kwamba imani ambayo Rais amekupa ni imani ambayo ni kubwa kwa mfano usalama uliopo, amani iliyopo, shughuli mbalimbali za kiuchumi wengi huwa wanasahau mchango mkubwa wa wasimamizi wa sheria na kwamba sheria zinafanyakazi ndio maana unaona kile ambacho kinaonekana,” amesisitiza.
Jaji Mkuu ameendelea kusema kuwa Mahakama itaendelea kuwapa ushirikiano wa hali ya juu kwa sababu mafanikio yao ndio mafanikio mhimili huo, kwa mfano “nikiangalia majukumu kwenye tovuti yenu ya kuendesha mashauri ya madai yakiwemo ya kikatiba, haki za binadamu kwa niaba ya Serikali ni eneo ambalo ni zito sana siku zote linawafanya kuwa na shughuli nyingi nchi nzima au kuratibu mashauri ya madai dhidi ya Serikali kwa kweli ninyi ndio watetezi wetu,”.
Halikadhalika amesema Mahakama au Bunge likishtakiwa ni wao ndio wanaenda mahakamani na kama kuna sheria ina changamoto yoyote pia wanashirikiana na mhimili huo kuijadili ili kuangalia namna bora ya kuboresha, hivyo kazi yao ni kubwa.
“Katika Mpango Mkakati wa Mahakama kuna dirisha la ushirikiano na wadau hilo dirisha siku zote lipo wazi na ndio maana linasaidia katika kuleta ushirikiano, kuna Msajili Mkuu wa Mahakama pamoja na Msajili wa Mahakama ya Rufani kwa upande wa utawala kuna Mtendaji wa Mahakama ya Rufani hawa wote ni viungo ambavyo vinaendeleza ule ushirikiano wa kila siku, Taasisi hizi mbili zina mambo mengi ya kujifunza kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hasa pale mnaposimamia kesi zenye uzito mkubwa,”amesema.
Jaji Mkuu amefafanua kwa kusema kuwa eneo jingine ambalo wanaweza kushirikiana katika akili bandia kati ya Mahakama, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, 0fisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ni kuwa taasisi hizo zinatengeneza taarifa nyingi ambazo zipo katika umiliki wao, hivyo jambo la kuangalia hivi sasa watazitumiaje kwa mfano kuna taarifa katika Mfumo wa Kitaifa unaochapisha taarifa za kisheria mtandaoni (TanzLII), kwenye tovuti zao na majalada yao yaliyo ya kijiditali yanawezaje kuhakikisha hizo taarifa zinaweza kuleta faida kubwa.
“Ni eneo ambalo tukijitenga hatuwezi kuwa na utafiti wa kudumu, lakini tukiwa na kikosi kazi ambacho kinajumuisha sekta zote za sheria na Mahakama ili ziweze kuangalia maendeleo ya akili bandia na namna gani yanavyogusa sheria zetu,” amesema.
Ametaja eneo lingine wanaloweza kufanya kazi kwa pamoja kwa kuwa tayari sheria nyingi zimetungwa na zinatoa nafasi ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, lakini matumizi yake bado yapo chini.
“Nadhani hili eneo tulifanyie mkakati wa pamoja ni namna gani tulazimishe kabla ya kuingia kwenye mapambano ya mashauri tutumie mifumo ya sheria ambayo inatutaka tuwe na maridhiano, majadiliano na upatanishi.Tayari kuna kada ya wapatanishi ambao wamesajiliwa kwanini hatutumii hizi njia ili tupunguze mashauri ambayo ni mengi yanatuchukulia muda wetu mwingi,”amesema.
Jaji Mkuu pia amegusia kuhusu elimu ya sheria (legal education) ambapo amesema elimu ya sheria ambayo inatokana na maudhui ya karne ya 20 na 19 inapaswa kuangaliwa kuwa inaendana na mahitaji na matarajio ya karne ya 21. Huku akitolea mfano kwamba ukiangalia mitaala ya vyuo vikuu bado inazungumzia mambo ya miaka ya 40.
Jaji Mkuu amesema kwamba siku hizi wanazalisha mawakili binafsi wengi na uwezo wa kiuchumi wa kuwapa ajira haupo, hivyo imefika wakati kuanza kuangalia shughuli za kiuchumi zianze kutoa ajira kwa wanasheria.
Naye Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Possi amesema asilimia 98 kazi zao zipo mahakamani na ni eneo muhimu kwa kujifunza na kupata maarifa. Pia amepokea ushauri wote kutoka kwa Jaji Mkuu na amesema atajitahidi kuhakikisha wataufanyia kazi kikamilifu ili kuhakikisha kuwa wanaisaidia nchi kikamilifu hasa katika eneo jipya la akili bandia.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wa (kwanza kushoto) akizungumza na Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Ally Possi (wa kwanza kulia na wadau wengine waliotembelea ofisi ya Jaji Mkuu wa Tanzania jijini Dar es Salaam.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Kiaki Nkya(wa kwanza kushoto) akizungumza jambo (wa pili kushoto) ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert na (watatu kushoto) ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bw. Victor Kategere wakiwa katika mazungumzo hayo.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati)akiwa katika picha ya pamoja Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Ally Possi(wanne kushoto), wakiwemo viongozi wengine Waandamizi wa Mahakama.
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni