Na INNOCENT KANSHA- Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa Viongozi wa Chama
cha Mawakili Tanganyika (TLS) kufanya kazi zao kwa kushirikiana na Serikali
kwani ndiyo nguzo kuu ya uwekezaji wa mambo yote makubwa katika shughuli zote za
kimaendeleo, ikiwemo sekta ya sheria.
Mhe.
Prof. Juma ametoa wito huo leo tarehe 26 Septemba, 2024 jijini Dar es Salaam alipokuwa
akizungumza na Kamati Tendaji ya TLS iliyomtembelea ofisini kwake na kuongeza kuwa hata nchi ya Marekani, ingawa inazungumzia umuhimu
wa sekta binafsi, ukienda mbali kimtizamo anayetayarisha mazingira ya
sekta binafsi ni Serikali.
“Serikali
ndiyo inaweka mazingira bora ya uwekezaji ikiwemo sekta ya sheria kwa kuweka
miundombinu rafiki ya kutekeleza majukumu yetu, mfano kujenga reli, barabara za
kisasa, viwanda vikubwa, bandari na mifumo imara ya
mtandao wa mawasiliano,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Jaji
Mkuu ameongeza kuwa sekta binafsi, ikiwemo ya sheria haiwezi kuja ikajenga reli, ikaweka
miundombinu rafiki ya mtandao wa mawasiliano na miundombinu mingine mingi bora inayosaidia kutoa huduma kwa wananchi. Hivyo, alitoe rai
wasiiweke Serikali mbali bali wahakikishe maswali yawe nafasi za ajira ikoje kwa vijana na wanasheria pale uwekezaji wowote unapojitokeza .
“Ukiangalia
kwa kweli Serikali ni mwekezaji mkubwa ambaye
tukimtumia vizuri anaweza kutusaidia, ukitazama miradi mikubwa yote anayefungua
njia ni Serikali ili sekta binafsi iingie. Sekta binafsi haiingii sehemu
ambayo ina hasara na haya maeneo makubwa yote ya kiuwekezaji yanatokana na
sekta binafsi. Mawakili mna nafasi ya kuongeza ujuzi na mafunzo ya kukabiliana
na teknolojia mpya ili muweze kuwa bora kitaaluma kwenye hizo nafasi za ajira
mpya,” ameongeza Mhe. Prof. Juma.
Aidha, Jaji Mkuu amefafanua kuwa, Kamati hiyo imepewa mamlaka ya kufanya mabadiliko
na mageuzi ya kisekta kwenye mambo makubwa na siyo madogo yatakayodumu muda mrefu katika maisha ya Mawakili.
“Baadhi
ya Mawakili wengine ni watoto wetu, changamoto wanazozipata wengi wetu tunaziona
nyumbani na tunanyang'anyana nao pesheni. Unakuta ana shahada, amesoma vizuri lakini
bado anategemea pesheni ya mzazi, wakati mzazi naye alitegemea aanze kupata
ruzuku kutoka kwake,” amesema Jaji Mkuu.
Mhe.
Prof. Juma akaongeza kuwa, wanapaswa kutafakari namna bora ya kutengeneza
maslahi na kuhakikisha wanafanikiwa kwa sababu milango ipo wazi siku zote na wakiwa na hoja zitapimwa na ushauri utatolewa wa kufikia malengo waliyojiwekea ili kuyafikia.
Jaji
Mkuu ameikumbusha Kamati hiyo kuwa, maboresho makubwa yaliyofanywa na yanayoendelea
kutekelezwa na Mahakama yanatokana na Mahakama kuisoma Dira ya Maendeleo
ya Taifa ya Mwaka 2025 na kuangalia Tanzania kama nchi inaenda wapi.
“Kwa
hivyo tunahakikisha shughuli zetu zote zinaendana na kutekeleza yale malengo ya
dira ya taifa na ndiyo maana utakuta tunapata unafuu wa kibajeti kutekeleza
majukumu yetu. Mahakama imekuwa ikijielekeza kwamba yenyewe ni sehemu ya
utekelezaji wa Dira ya Taifa,” ameongeza Jaji Mkuu.
Mhe.
Prof. Juma aliendelea kuwakumbusha kuwa Mpango Mkakati wa Mahakama umeweka
shabaha kwamba chochote kinachotekelezwa na Mahakama, mathatlani huduma ya
utoaji haki, haki za binadamu, utawala bora ni sehemu ya kufikia Dira ya Taifa
ya Mwaka 2025. Kwa hiyo, alisema Mahakama inatumia lugha ya kimaendeleo ili kujenga hoja
kupata fedha zinazotolewa kwenye shughuli za kiserikali.
"Mageuzi haya yametusaidia kupata
rasilimali fedha za kuweza kufanya maboresho, na mimi naamini chama
chenu ni wadau muhimu wa sheria. Nyinyi ndiyo chimbuko la wanasheria watakaoenda kufanya kazi za ushauri wa
matumizi ya sheria, hivyo tukiwapa msingi mzuri na mkiwezeshwa mtaweza kufanya
kazi ambayo itaisaidia jamii,” alisema.
Jaji
Mkuu akaongeza kuwa, ukiangalia maneno ya utangulizi ya Rais wa Awamu ya Tatu
Benjamin William Mkapa ya kwenye Dira ya Mwaka 2025, yalilenga kuangalia Tanzania
ya miaka 25, kwamba itakuwa ni Tanzania ya aina gani, kama unataka
kufanikiwa ukiwa mwanasheria au mwandishi ni vitu gani vya kuangalia. Alieleza kuwa utangulizi
huo unasema katika robo karne hiyo itatawaliwa na sifa ya ushindani, mfano kwenye ajira na kila kitu.
Alibainisha kuwa hakuna rasilimali zitakazowatosheleza watu wote na lazima kutakuwa na
ushindani kupata rasilimali hizo, ikiwa ni karne itakayo tawaliwa na wale wenye
uwezo mkubwa wa kutawala maendeleo ya sayansi na teknolojia. Mhe. Prof. Juma aliieleza Kamati hiyo kuwa eneo hilo ni
lazima Mawakili wajijenge katika uwezo wa matumizi ya teknolojia na matumizi ya
akili mnemba ili waweze kwenda sambamba na mageuzi hayo.
“Tunapozungumzia soko la Mawakili hatuzungumzii soko la mawakili Tanzania tu, tunazungumzia soko linalotokana na utandawazi na soko kutoka nje ambalo lina nafasi zaidi kuliko ndani ya nchi,” ameongeza Jaji Mkuu.
Kwa
upande wake Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface
Mwabukusi amesema Chama kupitia Kamati Tendaji wanaipongeza Mahakama ya
Tanzania kwa juhudi kubwa za kuendelea kutoa huduma zake
zinazoendana na karne ya 21.
“Miundombinu
bora ya kutolea huduma ya haki, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
ni kiashiria tosha kwamba wezentu mmepiga hatua kubwa na kutuacha kwa mbali, ubora huu ni wa kipekee,” amesema Rais Mwabukusi.
Rais Mwabukusi, kwa niaba ya Kamati Tendaji ya Chama hicho, akatoa baadhi ya maombi kwa Mahakama ya kurekebisha baadhi ya mambo yatakayowasaidia Mawakili kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Moja ya mambo hayo ni kuunganisha mfumo wa Mahakama wa kutambua Mawakili ili usomane na mfumo unatumiwa na Chama hicho ili waweze kubaini baadhi ya Mawakili wasiofanya vizuri katika kutoa ada zao za uwanachama, kwani Chama kinajiendesha kwa kutegemea michango ya Mawakili.
Rais huyo ameiomba Mahakama kupitia kwa Jaji Mkuu kutazama kwa karibu muundo wa mfumo wa sasa wa Kamati ya Maadili ya Mawakili, bila kuathiri mambo mengine, ili uwekewe utaratibu mzuri wa namna bora ya kusimamia nidhamu ya Mawakili.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akizungumza na Wajumbe wa Kamati Tendaji ya Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) (hawapo pichani) walipomtembelea ofisini kwake na kufanya mazungumza ya kina ya mambo mbalimbali ya maendeleo ya chama hicho leo tarehe 26 Septemba, 2024 jijini Dar es Salaam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni