• Atembelea Gereza la Wilaya Njombe
• Akagua Mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Njombe
• Azungumza na Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe
Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru amefanya ziara ya kutembelea Gereza la Wilaya Njombe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya za Mkoa wa Njombe aliyoanza kuanzia tarehe 23 hadi jana 26 Septemba, 2024.
Akiwa katika Gereza hilo, Mhe.Ndunguru alisomewa taarifa fupi kutoka kwa Mkuu wa Gereza SP. Jamhuri Njaidi ambaye aliipongeza Mahakama kwa kuendesha mashauri kwa wakati jambo ambalo limepunguza msongamano mkubwa wa wafungwa kutoka wafungwa 400 kwa miaka mitatu iliyopita mpaka kufikia jumla wafungwa na mahabusu 182 kwa sasa.
Akiwa ndani ya Gereza hilo, Jaji Mfawidhi huyo alisikiliza risala ya wafungwa ambao walitoa changamoto mbalimbali hasa ya umbali wa kusikiliza mashauri yaliyopangwa kwenye vikao vya Mahakama Kuu ambapo huwabidi kusafiri kutoka mkoani Njombe mpaka Mahakama Kuu Iringa. Wafungwa hao walipendekeza kuongezeka kwa idadi ya vikao vya Mahakama Kuu.
Katika tukio hilo, Mhe. Ndunguru aliwajibu kuwa, kwa Mkoa wa Njombe tayari kuna jengo linajengwa la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki, hivyo mashauri ya Mahakama Kuu na mashauri ya Mahakama ya Rufani yatakuwa yanasikilizwa kwenye Mkoa huo pindi ujenzi wa Mahakama hiyo utakapokamilika.
Aidha, changamoto nyingine zilizoibuka zilijibiwa palepale na wadau wa haki jinai waliokuwepo katika kutembelea Gereza hilo na ambazo hazijajibiwa, Mhe. Ndunguru alitoa siku tano changamoto hizo ziwe zimetatuliwa.
Katika muendelezo huo wa ziara yake Mhe. Ndunguru alitembelea pia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Njombe na kuonana na Katibu Tawala, Bi. Judica Omary na kuzungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka.
Katika Mazungumzo yao, Bi. Judica alimshukuru Jaji Mfawidhi kwa ujio wake na kumueleza kuwa, watashirikiana vizuri na Mahakama katika kutatua kero mbalimbali za wananchi huku kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Mahakama kwa kuwapa imani wananchi wa Mkoa wa Njombe.
Kadhalika, Jaji Mfawidhi huyo alitembelea Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Njombe na kukagua maendeleo ya ujenzi huo ambapo alipokea taarifa fupi ya Mradi huo kuwa, mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 28.
Akizungumza mara baada ya kukaguaa ujenzi huo aliwasisitiza wasimamizi wa Mradi huo kuongeza kasi ya ujenzi ili kukamilisha kwa wakati kulingana na makubaliano ya mkataba.
Kabla ya kuhitimisha ziara yake, Mhe. Ndunguru alizungumza na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe ambapo aliwasisitiza Mahakimu kuongeza kasi katika kupandisha mashauri kwenye Mfumo wa Usimamizi na Uratibu wa Mashauri (e-CMS).
Pamoja na hayo aliwasisitiza pia watumishi hao kufanya kazi kwa uadilifu na nidhamu sambamba na kuepuka vitendo vya rushwa vitakavyochafua taswira nzima ya Mahakama.
Jaji Mfawidhi aliongeza kwa kuwataka watumishi wa Mahakama hiyo kuwa na upendo wanapotimiza majukumu yao ya kikazi na kusema kwamba, “sisi tunaoshinda pamoja kuanzia asubuhi mpaka jioni kwenye jengo moja halafu tunakuwa tunachukiana sisi litakuwa si jambo jema maana tutashindwa kufikia lengo la mwajiri kwa kufanya kazi kwa ushirikiano kwa sababu ya chuki ya wenyewe kwa wenyewe.”
Kadhalika, Mhe. Ndunguru aliwasisitiza pia watumishi hao kujiendeleza kielimu na kuwataka kujiwekea ratiba ya kufanya mazoezi ya viungo ili kuweka vizuri afya zao.
Katika ziara hiyo, Jaji Mfawidhi aliambatana na Viongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe akiwemo Naibu Msajili, Mhe.Bernazitha Maziku, Mtendaji wa Mahakama Kuu Iringa, Bi. Melea Mkongwa, Hakimu Mkazi Mfawidhi Njombe, Mhe.Liadi Chamshama na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw.Richard Mbambe.
Jaji Mfawidhi huyo alitembelea Mahakama za Wilaya Ludewa, Makete, Wanging’ombe na kumalizia ukaguzi katika Wilaya ya Njombe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni