Ijumaa, 27 Septemba 2024

NAIBU WAZIRI KATIBA NA SHERIA ATEMBELEA KITUO JUMUISHI TEMEKE

  • Ashangazwa na maboresho makubwa yanayofanyika
  • Apongeza uongozi imara wa mahakama kwa kusimamia mageuzi hayo

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini jana tarehe 26 Septemba, 2024 alitembelea Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali na kujionea shughuli za kimahakama zinazotolewa kwa wananchi.

Mhe. Sagini aliwasilisha katika Kituo hicho saa 4.30 asubuhi na kupokelewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni, Bi. Mary Shirima, Naibu Msajili, Mhe. Frank Moshi na Mtendaji Mahakama Kuu Kituo Jumuishi Temeke, Bw. Samson Mashala.

Baadaye alipitishwa kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo ofisi ya Ustawi wa Jamii, Dawati la jinsia,chumba cha kunyonyeshea watoto na msaada wa kisheria kabla ya kukutana na Jaji Mfawidhi, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa kwa mazungumzo mafupi.

Mhe. Sagini baadaye alielekea kwenye ukumbi maalum na kupokea taarifa ya utendaji wa Kituo hicho iliyowasilishwa na Naibu Msajili. Katika taarifa yake, Mhe. Moshi alimweleza Naibu Waziri kuwaKituo hicho kilianzishwa kwa ajili ya kushughulikia au kusimamia na kuratibu jukumu la upatikanaji na utoaji wa haki kupitia usikilizaji wa mashauri ya mirathi na ndoa na kuyatolea maamuzi kwa wakati.  

Alieleza lengo lingine ni kuweka huduma za masuala ya familia katika Kituo kimoja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma zote ndani ya jengo moja na kimekuwa kinahudumia Mkoa mzima wa Dar es Salaam kwa usikilizwaji wa mashauri ya mirathi, ndoa na talaka pamoja na madai kwa mashauri ya Watoto.

Naibu Msajili alibainisha pia kuwa mbali na huduma za kimahakama, kuna ofisi za wadau kwa ajili ya kusogeza huduma kwa wananchi. Wadau wanaotoa huduma katika jengo hilo hadi kufikia mwezi Juni, 2024 ni Ustawi wa Jamii; WILAC; WiLDAF; LHRC; BAKWATA na Polisi Dawati la Jinsia. 

“Tangu kuanzishwa kwake hadi kufikia tarehe 31 Julai, 2024, Kituo kimeweza kuhudumia wateja wapatao 526,262, kati ya hao wanaume wakiwa 228,447, sawa na asilimia 43.4 na wanawake 297,815, sawa na asilimia 56.6 ya wateja wote waliopata huduma kwa kipindi chote,” alisema.

Mhe. Moshi alimweleza Naibu Waziri pia kuwa Kituo kimefanikiwa kusajili na kuamua mashauri ya kifamilia katika ngazi zote za Mahakama. Kwa mwaka 2021 Kituo kilisajili jumla ya mashauri 2,383 na kuamua mashauri 1,166 na kubaki mashauri 1,217. 

Alieleza kuwa mwaka 2022 yalisajiliwa mashauri 8,554, yaliamuliwa mashauri 7784 na yakabaki 1987 na mwaka 2023 yalifunguliwa mashauri 8,279 na kuamuliwa mashauri 8,676 na yaliyobaki mashauri 1590. 

“Kipindi cha mwezi Januari 2024 hadi mwezi Julai 2024, Kituo kimesajili jumla ya mashauri 4,993. Mashauri 4,131 yameamuliwa na jumla ya mashauri 2,452 yalibaki… 

“…Takwimu hizi zinaonesha Kituo kinasajili idadi kubwa ya mashauri kila mwaka. Hata hivyo takwimu zinadhihirisha kuwa ipo haja kwa wananchi na wadau kutilia mkazo suala la usuluhishi katika kushughulikia masuala ya familia,"alisema. 

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni alimweleza changamoto ambazo zinakikabili Kituo katika uendeshaji wa mashauri ya familia, ikiwemo ucheleweshaji wa wananchi kuhamisha mali za marehemu kwenda kwa warithi na jamii na wadau kutokuwa na uelewa wa kutosha  juu ya masuala ya mirathi na  ndoa. 

“Changamaoto nyingine ni wananchi kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa uandishi wa wosia. Kesi nyingi za mirathi zinazofunguliwa hapa kituoni ni zile ambazo Marehemu hakuacha wosia. Zipo pia baadhi Marehemu ameacha wosia wa jinsi gani mali zake zigawiwe baada ya kufa kwake na kwa watu gani,” alisema.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mhe. Sagini aliupongeza uongozi wa Mahakama ya Tanzania, chini ya Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kusimamia mageuzi makubwa yanayoonekana mahakamani kwa sasa.

“Tumshukuru Jaji Mkuu kwa kuwa kinara kwenye maboreshio haya. Tungeweza kuwa na maboresho ya miundombinu, tukaongeza Majaji, lakini kama hakuna utashi wa mkuu wa Mhimili tungekwama. Ukiona Mkuu wa Mhimili anasimamia mabadiliko haya lazima tutafanikiwa…

“Mmesimamia vizuri sana fedha ambazo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliridhia na Bunge kupitisha na kuletwa kwenye Mhimili huu. Niwapongeze kwa kazi hii nzuri mliyofanya, ukiangalia uwekezaji huu na thamani ya fedha iliyotumika na mkabakisha fedha baada ya mradi kukamilika,” alisema.

Naibu Waziri alieleza kuwa ameshuhudia maboresho makubwa ambayo yanaendelea kufanyika ndani ya Mahakama ya Tanzania ili kuboresha huduma za utoaji haki, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya majengo na mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

“Nilitembelea pale Dodoma nimeona maboresho makubwa sana yaliyopo katika Mhimili wa Mahakama Tanzania. Ninaamini watu waliohudumu mahakamani miaka ile, leo wanajiona wapo zaidi ya Ulaya. Haya ni mambo makubwa ambayo kama nchi tunapaswa kujivunia kuwa tumeyafanya sisi wenyewe kama Watanzania,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuviomba vyombo vya habari kutangaza maboresho hayo makubwa kwa wananchi ili wajue kinachoendelea katika Mhimili wa Mahakama na hatua nyingi zilizochukuliwa katika kuboresha na kuweka mazingira wezeshi kwenye utoaji wa haki.

Naye Mtendaji Mkuu alibainisha kuwa jitihada za Mahakama ya Tanzania kuboresha huduma za utoaji haki ni endelevu na kwamba mbali na Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita ambavyo vimeshajengwa, Mahakama inatekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2020/2021-2024/2025) awamu ya pili. 

Alisema kuwa jumla ya Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo 60 zinajengwa na Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki tisa vinajengwa katika Mikoa ya Katavi, Songwe, Njombe, Songea, Lindi, Geita, Simiyu, Singida na Visiwani Pemba.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini (juu na chini) akipokelewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama alipowasili katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kwa ziara fupi.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini (aliyenyoosha mikono) akisalimiana na sehemu ya wananchi waliofika kupata huduma katika Kituo hicho. Picha chini akimpa zawadi mtoto katika Chumba cha Kunyonyeshea kilichopo katika Kituo hicho.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini akipata maelezo kutoka kwenye Chumba cha Msaada wa Kisheria. Picha chini akiwa katika Chumba cha Ustawi wa Jamii.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akieleza jambo kabla ya Naibu Waziri kuhitimisha ziara yake.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini (juu na chini) akifafanua jambo alipokuwa anazungumza wakati wa ziara yake.


Naibu Msajili, Mhe. Frank Moshi akifafanua jambo alipokuwa anawasilisha taarifa ya utendaji wa Kituo hicho kwa Naibu Waziri (hayupo kwenye picha).

Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni, Bi. Mary Shirima akieleza changamoto kadhaa wanazokabiliana nazo kwenye Kituo hicho wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali. Wengine waliokaa ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni, Bi. Mary Shirima. Picha chini, Viongozi hao wakifurahia jambo.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini (juu na chini) akiagana na Viongozi wa Mahakama baada ya kuhitimisha ziara yake.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni