- Yazuia
Mahakimu kuhamia Taasisi nyingine
- Ni
baada ya kuwapika na kuwa wanasheria bora
Na MAGRETH KINABO NA INNOCENT
KASHA- Mahakama, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi ya Mahakama, ambaye
pia ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma ametoa msimamo wa Tume kuwa haitawachia Mahakimu wake kwenda
kufanya kazi mahali pengine, kwa sababu tayari Mahakama imeshawajenga na
kuwapika ili waweze kutoa huduma ya utoaji haki kwa ubora na ufanisi.
Aidha, Mwenyekiti huyo, amewataka watu wengine
wanaowahitaji Mahakimu hao, kuiga mfano wa Mahakama ya Tanzania wa
kuwaajiri wanasheria wengine wasio na ajira, na kuwajengea uwezo na kuwapika.
Uamuzi huo umetolewa leo tarehe 20 Septemba, 2024 na
Mwenyekiti, huyo wakati akitoa hotuba yake mara baada ya kuwaapisha
Mahakimu Wakazi wapya 22 wa Mahakama za Mwanzo, kwenye hafla iliyofanyika
katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia (IJC),kilichopo Temeke jijini Dar
es Salaam.
“Kwa hiyo sisi tunapowachukua hatuna nia ya
kuwaachia. Watakuja watu wengine wenye mishahara zaidi
watasema tunataka hakimu fulani, hatuwapi tunawambia wao wawe na
mipango ya kuwa na wanasheria ambao wapo wengi, ambao hawana ajira na
wanasubiri ajira wawachukue na kuwapa mafunzo na kuwatengeneza wakawe wenyeviti
wa mabaraza ya ardhi.
“Kwa hiyo tuelewane tunawachukua hatuna talaka,
sisi hatuachani na ninyi, Huu ndio msimamo wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa
haitawachia wafanyakazi bora,” amesema Mhe. Prof. Juma.
Mwenyekiti huyo, alisema Mahakama iko tayari kutoa
mafunzo kwa wanasheria hao, watakaoajira na watu wengine kupitia Chuo Cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) au kusaidia kuwafundisha kupitia Majaji au
Mahakimu wenye uzoefu.
Mhe. Prof. Juma alisema mfumo wa
ajira wa Mahakama ni wa kujitahidi kuwajenga mahakimu ili waweze kutoa huduma
bora zaidi.
“Sisi tunawajenga kimaadili na kiuwezo na ndio maana mchakato wa kuwapata Mahakimu unachukua muda mrefu,”amesisitiza Mwenyekiti huyo.
Akizungumzia kuhusu uendeshaji na usimamizi wa
shughuli za kimahakama, alisema majukumu ya Mahakimu
hao yameainishwa kwenye Katiba, Sheria na Kanuni mbalimbali. Ibara
ya 107A (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano (1977) inawaelekeza Mahakimu na
Majaji kufanya maamuzi ya mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria.
Hivyo Ibara hiyo inakwenda mbali zaidi kwa kuwataka
kuzingatia pia misingi kadhaa za utoaji haki,ambayo ni kutenda haki kwa wote
bila ya kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi. Pili kutochelewesha haki bila
sababu ya kimsingi. Tatu, kuamuru fidia ipasayo kwa watu wanaoathirika
kutokana na makosa ya watu wengine, na kwa mujibu wa sheria mahsusi iliotungwa
na Bunge.
Nne kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya
wanaohusika katika migogoro. Tano, kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na
masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka.
Hata hivyo, aliongeza kwamba kazi ya Jaji au
Hakimu ni huduma kwa binadamu. Maamuzi, hukumu na amri zenu Mahakimu ni lazima:
ziwe zinaeleweka, zinatekelezeka, zinatatua
migogoro na zinajibu hoja zilizoletwa mahakamani.Upande utakaoshinda lazima
ufahamu sababu za kushinda, na upande utakaoshindwa upewe sababu kwa nini
umeshindwa.
Akielezea kuhusu uzito wa kiapo cha Hakimu, alisema kinakukumbusha
wajibu mzito uliopewa naJamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Kazi ya Uhakimu.
Hivyo kiapo cha Uhakimu ni sehemu ya Utumishi wao kwani kinawakumbusha
kuwa wanatakiwa kufanya kazi kwa uaminifu mkubwa, bila upendeleo wowote na kwa
kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni za Maadili za Maafisa Mahakama.
“Mahakimu jihadharini kukiuka Maadili kwa
kujihusisha na kutoa ushauri kuhusu mashauri yaliyo mbele ya Mahakimu Wenzenu.
Jihadharini na ndugu, jamaa, marafiki wenye mashauri mahakamani ambao
watawatembelea nyumbani kuwasimulia lakini kwa lengo la kupata ushauri au
kukuvuta uwakosoe Mahakimu wenzako kuhusu shauri linaloendelea Mahakamani,”
amesema.
Halikadhalika Mwenyekiti huyo, aliwaasa Mahakimu
hao kufahamu kuwa miongozo ya MahakamaKuu na Mahakama ya Rufani imerahisishwa
na urahisi wa kuzisoma hukumu zinazopandishwa katika mfumo wa TANZLII. Hivyo
hakuna sababu ya kukosea kwenye maamuzi kwani miongozi inapatikana kwa urahisi.
Kwa sasa hata kama huna mtandao unaweza kupata
maamuzi ya TANZLII kupitia mpango wa Sheria Mfukoni (POCKET LAW) ambao
unakuwezesha kupata maamuzi ya TANZLII hata ukiwa huna mtandao.
Wakizungumza kwa niaba ya wengine, Mahakimu James
Kapele na Kuruthumu Said Mkundawatu, wamesema wanashukuru kufikia hatua hiyo na
kuahidi kutoa haki kwa wananchi kwa wakati.
Mahakimu hao watapatiwa mafunzo elekezi kuanzia
Septemba 23, 2024 hadi Oktoba, 2024. Lengo mafunzo hayo ni kuwawezesha Mahakimu
wapya kuielewa Mahakama pamoja na utamaduni wake na misingi yake.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi ya Mahakama, ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hutoba mbele ya Mahakimu Wakazi Wapya 22 (hawapo pichani) walioapishwa leo tarehe 20 Septemba, 2024 katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia -Temeke jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi ya Mahakama, ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitia saini hati ya kiapo cha Hakimu Mkazi mara baada ya kumuapisha.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi ya Mahakama, ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimwapisha Hakimu Mkazi Mpya Mhe. Lilian James Kombe wakati wa hafla ya uapisho wa Mahakimu wakazi 22 ulifanyika jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi ya Mahakama, ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitia saini hati ya kiapo cha Hakimu Mkazi Mhe. Kuruthum Said Mkundawatu mara baada ya kumuapisha.
Sehemu ya Mahakimu Wakazi wapya 22 wa Mahakama za Mwanzo wakifuatilia hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi ya Mahakama, ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani), kwenye hafla iliyofanyika katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia (IJC),kilichopo Temeke jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya jopo la Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania likiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (wa kwanza kulia) wakifuatilia hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi ya Mahakama, ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani), kwenye hafla iliyofanyika katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia (IJC),kilichopo Temeke jijini Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni