- Pongezi hizo zinatokana na Mahakama Kuu Jijini Mbeya kupokea Mahakama Inayotembea
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa jitihada kubwa za kuboresha huduma za kimahakama ili kuhakikisha huduma za utoaji haki zinaendelea kumlenga mwananchi wa kawaida.
Akizungumza hivi karibuni katika hafla fupi ya kupokea gari maalum litakalotumika kama Mahakama Inayotembea ‘Mobile Court’, hafla iliyojumuisha na mafunzo kwa watumishi ya namna ya kutoa huduma kwa mteja katika Mahakama Inayotembea. Mhe. Tiganga alisema Mahakama hiyo itakuwa msaada mkubwa wa kuhakikisha huduma bora za kimahakama zinaendea kutolewa kwa wepesi na haraka bila kuathiri taratibu za utoaji haki kwa wananchi mahali popote walipo na kupunguza gharama za kuitafuta haki.
“Nitumie nafasi hii kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa jitihada kubwa inayoweka katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyo bora na tunaahidi kuendelea kutoa huduma iliyotukuka kwa wananchi kwa kuzingatia ufanisi na weledi mkubwa” alisema Mhe. Tiganga
Mapokezi hayo ya Mahakama Inayotembea yaliambatana na mafunzo ya namna ya uendeshaji wa huduma katika Mahakama hiyo, ambapo washiriki walikua ni Mahakimu wa Mahakama za Wilaya na Mwanzo, Maafisa usafirishaji, Maafisa Kumbukumbu pamoja na Afisa TEHAMA.
Aidha, wahusika wote katika mafunzo hayo walipewa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania unaotekeleza shughuli za Mahakama ikiwemo zile za Mahakama Inayotembea, ikiwa ni pamoja na Utawala, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali, upatikanaji na utoaji huduma kwa wakati, kuimarisha Imani ya Umma na kushirikisha wadau wakiwemo Viongozi wa Serikali za Mitaa, Polisi, Magereza pamoja na jamii kwa ujumla.
Naye, Mkufunzi wa mafunzo hayo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Moses Ndelwa akifafanua juu ya nguzo zinazosimamia Mahakama Inayotembea alisema kuwa, lengo ni kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na jamiii, kuongeza ufanisi na weledi katika utoaji haki na usikilizwaji wa mashauri mbalimbali na pia kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi kwa kutumia Mahakama Inayotembea itapunguza gharama za wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kimahakama na kuokoa muda.
“Ni muhimu kwa watoa hudumu katika Mahakama Inayotembea kuepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kuongeza imani kwa wananchi. Aidha kupitia mpango huu wa Mahakama Inayotembea Tanzania imepata sifa kubwa sana kimataifa, mpaka kupelekea baadhi ya mataifa ya Afrika kuja kujifunza jinsi ya uendeshaji wa Mahakama hizi, baadhi ya mataifa hayo ni Ethiopia, Uganda na Malawi na Zimbabwe,” alisisitiza Mhe. Ndelwa
Aidha,
shabaha kubwa ya Mahakama Inayotembea inalenga kuongeza wigo wa kutoa huduma za
haki kwa wananchi kwa kuwafikia watu 5,833 kwa mwaka na kusikikiliza mashauri
kwa wakati, kwa muda usiozidi siku thelathini (30) kwa shauri lililosajiliwa,
kutoa huduma zenye ubora, kutoa ratiba za vikao, kutoa elimu kwa umma, kukuza
matumizi ya teknolojia na kutoa taarifa mbalimbali za mashauri yaliyoamuliwa
kwenye Mahakama Inayotembea kwa haki na kwa wakati.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni