Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi amewataka Mahakimu wa Mkoa huo kujifanyia tathmini ya namna ya usikilizaji wa mashauri kwa kutumia Mfumo wa Kieletroniki wa Kuratibu Mashauri (e-CMS) ambao kwa sasa una takribani miezi kumi tangu uanze kufanya kazi.
Akitoa hotuba ya kufungua kikao cha Menejimenti jana tarehe 05 Septemba, 2024 kilichofanyika katika Hoteli ya Mark iliyopo wilayani Mkuranga, Mhe. Mkhoi aliwasisitiza Mahakimu Wafawidhi kuendelea kubainisha changamoto wanazokabiliana nazo katika kutumia Mfumo huo katika Mahakama zao.
“Nawasihi Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya kuwasimamia vyema Wafawidhi wa Mahakama za Mwanzo ili waweze kuingiza mashauri katika Mfumo wa Mahakama za mwanzo lakini pia kuwa na utaratibu wa kukagua mara kwa mara Mfumo wa kusajili mashauri ya Mahakama za Mwanzo ili kuweza kutoa mashauri ambao yameisha ili kusionekane kuna mlundikano wa mashauri katika Mahakama zetu,” alisema Mhe. Mkhoi.
Akizungumzia kuhusu Mahakama zote hasa za Mwanzo, Mfawidhi huyo aliwakumbusha kuhusu suala la kufunga mashuri ya Mirathi kwa wakati ambapo amewataka Wafawidhi wote kusimamia na kuwakumbusha Mahakimu wote kuzingatia na kuwaambia Wasimamizi wa Mirathi kufunga mirathi baada ya muda kutimia ili kuondokana na mlundikano wa mashauri.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama kwa mujibu wa Mpango Mkakati wa Mahakama kwa kipindi cha kuanzia tarehe 01 Julai, 2023 hadi Juni 2024 katika kikao hicho, Afisa Tawala wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bi. Stumai Hozza alisema kwa upande wa utawala bora ilibainisha kuwa, Mahakama za Mkoa wa Pwani zinasimamia shughuli za utoaji haki na utawala kwa jumla ya Mahakama za Mwanzo 39 na Mahakama za Wilaya saba (7) na hili limethibitika katika eneo la utekelezaji wa maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Mahakama, ukaguzi wa majalada ya rufaa na mapitio katika Mahakama za Wilaya.
Kadhalika, alisema utekelezaji wa Waraka Na. 4/2022 wa Jaji Mkuu unaohusu upangaji wa mashauri kwa kuzingatia muda, utekelezaji unafanyika ambapo mashauri yanapangwa kwa muda na wateja wanafika kwa muda waliopangiwa.
“Utoaji wa huduma bora katika Mahakama na wananchi wanapata huduma katika Mahakama zote za Mkoa wa Pwani kulingana na taratibu zilizopangwa, pia usikilizaji wa mashauri kupitia video unafanyika japo kuna changamoto ya mtandao,” alisema Bi. Stumai.
Katika utekelezaji wa Nguzo namba mbili (2) ya Mpango Mkakati inayosema Utoaji Haki kwa Wakati, alisema Mahakama Pwani inapokea, kusikiliza na kutolea uamuzi mashauri mbalimbali kwa mujibu wa sheria.
“Umalizaji wa mashauri kwa wakati umekuwa ukifanyika kwa ufanisi na weledi wa kutosha na kusababisha kupunguza malalamiko ya wananchi ya kucheleweshwa kwa mashauri. Mashauri yamekuwa yakisajiliwa kwenye Mfumo na kuhuishwa kwa wakati hali inayowezesha taarifa hizo za mashauri kupatikana kwa urahisi katika Mfumo wa e-CMS,” alieleza Bi. Stumai.
Aliongeza kuwa, katika kipindi cha mwaka 2023/2024 Mahakama ya Hakimu Mkazi ilifungua jumla ya mashauri 118 na kusikiliza mashauri 95 na kubakiwa na mashauri 56 na kwamba kasi ya umalizaji wa mashauri (Disposal rate) ni asilimia 63. Kwa upande wa Mahakama za Wilaya Pwani alisema yalifunguliwa mashauri 2,043 na jumla ya mashauri 2,232 yalisikilizwa na kubakiwa na mashauri 451 kwa mwezi Juni 2024.
“Kwa upande wa Mahakama za Mwanzo kwa mwaka 2023/2024 mashauri yaliyofunguliwa ni 7,054 na kusikilizwa mashauri 6782 kwa Mahakama zote za Mwanzo,” alieleza.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni