Jumatatu, 23 Septemba 2024

MAHAKIMU WAFAWIDHI KANDA YA MBEYA WAPIGWA MSASA

Na Daniel Sichula- Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga aliongoza kikao kazi cha Mahakimu Wakazi kutoka Mahakama za Mwanzo, Wilaya na mikoa ya Mbeya na Songwe ili kuleta uelewa wa pamoja katika kutekeleza msingi wa majukumu yao ya utoaji wa haki kwa wananchi.

Akizugumza mara baada ya kuwasilisha taarifa mbalimbali za utendaji kazi katika kikao kazi hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya hivi karibuni, Mhe. Tiganga alisema Mahakimu wengi wanatabia ya kuzichukulia kesi za mirathi kama vile ni kesi za kawaida ni muhimu sheria zinazoongoza mashauri hayo zifuatwe kwa kuzingatia umakini mkubwa kwa mdaawa yeyote ataekiuka sheria zilizopo.

“Ni jukumu la Mahakama kuwatafuta wadaawa wote ambao wanavunja sheria za mirathi na pia Mahakama inawajibu wa kupunguza muda wa kushughulikia stahiki za wanufaika wa mirathi husika ili kuondoa malalamiko,” aliongeza Mhe. Tiganga

Mhe. Tiganga aliongeza kuwa, mashauri ya madai yana changamoto nyingi, akawakumbusha Mahakimu wanapotoa hukumu za mashauri hayo wanapaswa kuwa makini sana na kuhakikisha malipo yote ya madai yanafanyika kwenye akaunti ya Mahakama.

Akizungumzia suala la uandishi wa hukumu Mhe. Tiganga alisema uandishi wa hukumu ni lazima uoneshe sababu za msingi za zisizo acha mashaka ili kumtia mtuhumia hatiani na pasipo kuwa na sababu hukumu hiyo inakuwa batili.

Kwa upande wake Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe Aziza Temu aliwakumbusha Mahakamu kuweka uataratibu wa kujikagua na kujitathimini wenyewe na zoezi hilo liendane sambamba na kuhuisha mashauri yanyoendelea na kumalizika mahakamani.

Naye, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Judith Lyimo aliwasisitiza wajumbe wa kikao kazi hicho kuendelea kuwajibika kwa bidii kulingana na miezi iliyobaki kabla ya mwaka kuisha kuhakikisha mashauri yote yanamalizika na kuepuka kuzalisha mlundikano.

Katika kuwasilisha taarifa, kikao kazi hicho kilisoma taarifa mbalimbali zikiwemo za utendaji kazi wa Mahakama hizo katika maeneo ya usajili wa kesi, upokeaji, utunzaji wa vielelezo, uendeshaji wa kesi za mirathi na madai, uandishi wa hukumu, utoaji wa nakala za hukumu kwa wadaawa na washitakiwa na taarifa za mahabusu.

Aidha, wajumbe waliohudhuria kikao kazi hicho, walimshukuru Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga, Naibu wasajili Mhe. Aziza Temu na Mhe. Judith Lyimo kwa kuandaa kikao kazi hicho kwani kilikuwa jukwaa zuri la kuwasaidia na kuwakumbusha mambo mengi ya kisheria mathalani uandaaji wa taarifa za utendaji wa haki kwa kufuata sheria ikiwa ni pamoja na misingi ya uandishi wa hukumu.

Akifunga kikao kazi hicho Mhe. Tiganga aliwashukuru Mahakimu hao na kuwambusha mambo ya msingi katika kusimamia haki kwa kufuata sheria, kuzingangatia weledi katika utendaji kazi, uadilifu pamoja na kufanya kazi kwa moyo wa kujitolea.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akifafanua jambo wakati wa kikao kazi cha Mahakimu Wakazi kutoka Mahakama za Mwanzo, Wilaya wa mikoa ya Mbeya na Songwe katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu jijini Mbeya.

Sehemu ya Mahakimu Wakazi kutoka Mahakama za Mwanzo, Wilaya wa mikoa ya Mbeya na Songwe katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu jijini Mbeya wakifurahia jambo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akifungua kikao kazi cha Mahakimu Wakazi kutoka Mahakama za Mwanzo, Wilaya wa mikoa ya Mbeya na Songwe katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu jijini Mbeya.


Meza Kuu ikiongozwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi kutoka Mahakama za Mwanzo, Wilaya wa mikoa ya Mbeya na Songwe.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha- Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni