Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kigali
Majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania wamechaguliwa kuwasilisha mada katika maeneo mbalimbali katika Mkutano wa Kimataifa wa Chama cha Majaji na Mahakimu kutoka Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini hapa.
Majaji hao ni Mhe. John Kahyoza, ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara na Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), ambaye atawasilisha mada kuhusu, “jinsi ya kuzuia uchafuzi wa mazingira unaovuka mipaka” kesho tarehe 9 Septemba, 2024.
Siku hiyo majira ya alasili, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta atawasilisha mada kuhusu, “utoaji wa adhabu kwenye kesi za utoroshaji wa wanyamapori.”
Mwingine ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi ambaye atawasilisha mada kuhusu, “upokeaji wa ushahidi unaotokana na kompyuta” majira ya alasili siku ya Jumatano tarehe 11 Septemba, 2024.
Mada zote tatu zitajadiliwa na Majaji wengine kutoka mataifa mbalimbali duniani. Wapo majaji kutoka mataifa mengine watawasilisha mada mbalimbali wakati wa Mkutano huo ambao unatarajiwa kufunguliwa rasmi wa Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame.
Kuchaguliwa kwa Majaji kutoka Tanzania kuwasilisha mada katika Mkutano huo kunatokana na jinsi Mahakama ya Tanzania ilivyopiga hatua kubwa kwenye maeneno mbalimbali, ikiwemo matumizi ya hali ya juu ya teknolojia katika shughuli za kimahakama.
Mapema asubuhi leo tarehe 8 Septemba, 2024, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameshiriki kwenye Mkutano wa Majaji Wakuu kutoka kwenye Jumuiya ya Madola, kuzungumzia mambo mbalimbali ya kimahakama.
Ujumbe kutoka Mahakama ya Tanzania unaoongozwa na Mhe. Prof. Juma uliwasili jana tarehe 7 Septemba, 2024 nchini Rwanda kushiriki Mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa Kigali.
Katika Mkutano huo, Jaji Mkuu ameongozana na Majaji wawili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Barke Sehel, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.
Wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani na Majaji wengine wa Mahakama Kuu, Mhe. John Kahyoza, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), Mhe. Ilvin Mugeta, Mhe. Butamo Philip, Mhe. Yohana Massara na Mhe. Dkt. Adam Mambi.
Viongozi wengine ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert, Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi, Katibu wa Jaji Kiongozi, Mhe. Aidan Mwilapwa na Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Dkt. Jovin Bishanga.
Wapo pia Viongozi wa JMAT, Mhe. Shaibu Mzandah, Mhe. Lazaro Magai, Mhe. Nemes Mombury, Mhe. Adeline Kashura, Mhe. Mary Kallomo na Mhe. Devota Ksebele na Mhe. Hassan Chuka ambaye pia ni Katibu wa Msajili wa Mahakama ya Rufani.
Mkutano huo wenye kauli mbiu ya “Haki Mazingira” umeandaliwa na Jumuiya ya Madola kwa kushirikiana na Mahakama ya Rwanda.
Katika Mkutano huo, Majaji na Mahakimu watajadili vipengele mbalimbali vya kisheria na kitaasisi ili kuimarisha usimamizi na upatikanaji wa haki kuhusiana na mazingira na jukumu kuu la Mahakama katika kudumisha haki mazingira.
Kupitia mada na mijadala mbalimbali, wajumbe wa Mkutano huo watakuwa na fursa za kubadilishana uzoefu kati yao na kuunda uhusiano wa kudumu miongoni mwao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni