Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim, Hamis Juma leo tarehe 7 Septemba, 2024 amemuapisha
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari kuwa Kamishna wa Tume hiyo.
Akizungumza baada ya kumuapisha Kamishna huyo, Jaji Mkuu wa
Tanzania alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa ushirikiano kwa Mahakama
ya Tanzania pamoja na taasisi nyingine na pia kushiriki kwenye vikao mbalimbali
vya Tume ya Utumishi wa Mahakama.
“Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kiungo muhimu katika
kuunganisha Mihimili ya nchi, hivyo sisi kwa upande wetu wa Mahakama
tunamtegemea sana katika kututetea na kutusemea kwenye masuala mbalimbali
yanayohusu Mahakama, alisema”.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu alimshukuru aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Feleshi kwa kazi kubwa aliyofanya na kwa
mchango aliotoa alipokuwa Kamishna wa Tume kwa kipindi cha miaka sita.
”Umekuwa daraja muhimu sana ambapo umetuunganisha sisi na
mihimili mingine, lakini pia ulishiriki vikao na ziara za Tume licha ya
majukumu mengine makubwa uliyokuwa nayo, tunakushukuru sana”, alisema Jaji Mkuu.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa kuwa Kamishna wa Tume
ya Utumishi wa Mahakama, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameahidi kutoa
ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Tume.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwaahidi kuwa Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu itachukua nafasi yake stahiki na kutoa mchango wake ipasavyo
katika katika shughuli za Tume na kuhakikisha kwamba tunakuwa daraja zuri kwa Mihimili
ya nchi katika kutekeleza majukumu yake” alisema.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
na Kamishna ya Tume ya Utumishi wa Mahakama aliyemaliza muda wake Jaji wa
Mahakama ya Rufaa Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi amemuasa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kuendeleza ushirikiano na Tume na kuisaidia inatekeleza majukumu yake.
Kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Utumishi wa Mahakama
inaundwa na wajumbe wafuatao; Jaji Mkuu ambaye ni Mwenyekiti, wajumbe wengine
wa Tume ni Mwanasheria Mkuu wa Serikal, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani ambaye anateuliwa na Rais, pamoja na
wajumbe wawili wanaoteuliwa na Rais. Aidha, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania ni Katibu wa Tume na ndiye mtekelezaji wa maamuzi yote ya Tume.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo
cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim, Hamis Juma akimuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari kuwa Kamishna wa Tume hiyo leo tarehe 7 Septemba, 2024 jijini Dar es salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni