Alhamisi, 12 Septemba 2024

WATENDAJI WA MAHAKAMA WAKUTANA KUJADILI UBORESHAJI UTENDAJI KIMKAKATI

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

Watendaji wa Mahakama nchini Tanzania jana tarehe 11 Septemba, 2024 walikutana mkoani Morogoro kwa ajili ya kikao kazi ili kukumbushana mambo mbalimbali yanayolenga kuboresha na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kiutendaji. 

Akizungumza wakati wa kufungua kikao kazi hicho Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel alisema lengo la kikao kazi hicho ni kuhakikisha watendaji wote wa Mahakama ya Tanzania wanajengewa uelewa wa pamoja wa namna bora ya kusimamia kwa ufanisi majukumu yao wakati wanapotekeleza shughuli za kiutawala ndani ya Mahakama.

Aliongeza kuwa, Mahakama inatambua kwamba kuna Watendaji ambao wametoka katika nyadhifa mbalimbali kabla ya kushika nyadhifa za utendaji ndani ya Mahakama hivyo mafunzo hayo yatawajengea ufanisi mzuri wa namna ya kutekeleza majukumu ya kiutendaji ndani ya Mahakama. 

Aidha, Prof. Ole Gabriel alisisitiza kwamba kikao kazi hicho kitakapo hitimishwa kitakuwa kimewajengea Watendaji hao mawazo chanya na ya kimkakati katika kushughulikia mambo yote ya kiuongozi na kiutendaji na kusimamia kwa ukamilifu Mpango Mkakati wa Mahakama unaondelea kutekelezwa.

“Ni matumaini yangu na ya Mahakama kwa ujumla kwamba mara baada ya kikao kazi hiki tutakuwa na watendaji wa Mahakama ambao utendaji kazi wao utakuwa wa kutanguliza maslahi ya kitaasisi katika kumuhudumia mwananchi wa kawaida anayetafuta haki Mahakamani na hili litawezekana iwapo tutafanya kazi kama timu moja,” alieleza Prof. Ole Gabriel.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Bw. Leonard Magacha akitoa neon la utangulizi kabla ya kufungua kikao kazi hicho aliwakumbusha washiriki wote waliopo kwenye mkutano huo watambue kuwa wao ndiyo wasaidizi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama hivyo kufanikiwa kwa Mtendaji Mkuu kunawategemea wao katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa.

Naye, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania Bi. Beatrice Patrick alisema kuwa kikao kazi hicho kimewashirikisha washiriki thelathini na tisa (39) ambao ni watendaji toka Kanda za Mahakama na Divishini zote Tanzania. Aliongeza kuwa, mada zitakazotolewa ni pamoja na namna bora ya kusimamia utawala katika maeneo ya kazi, kukumbushana utamaduni wa Mahakama, kupeana ujuzi wa kuongeza ufanisi katika majukumu ya kazi na kuelekezana namna ya uendeshaji wa mashauri ya nidhamu kwa watumishi wasio Maafisa Mahakama. 

Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu anayesimamia Divisheni Bi. Mary Shirima alisema kuwa anaamini kuwa mara baada ya mafunzo hayo watendaji watashusha elimu hiyo kwa watumishi walioko chini yao kwa lengo la kuleta uelewa wa pamoja kwa watumishi wa Mahakama. 

Kikao kazi hiko ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa Mwaka 2020/2025 ambao miongoni mwa nguzo zake ni Pamoja na kuboresha uwajibikaji, uwazi na matumizi ya Tehama kinategemewa kufanyika kwa muda wa siku nne kuanzia leo tarehe 11 Septemba, 2024 hadi tarehe 14 Septemba, 2024.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa hotuba wakati akifungua kikao kazi cha watendaji wa Mahakama nchini Tanzania jana tarehe 11 Septemba, 2024 kinachofanyika mjini Morogoro.

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania Bi. Beatrice Patrick akitoa ufafanuzi wa lengo la kikao kazi hicho.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Bw. Leonard Magacha akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi aweze kuzungumza na Watendaji hao.

Meza Kuu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya watendaji wa Mahakama ya Tanzania wanaoshiriki kikao kazi hicho mjini Morogoro.

Sehemu ya watendaji wa Mahakama ya Tanzania wanaoshiriki kikao kazi hicho mjini Morogoro wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa mgeni rasmi Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani).

Meza Kuu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania wanaoshiriki kikao kazi hicho mjini Morogoro.

(Habari Hii imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni