Na FAUSTINE KAPAMA, Mahakama ya Tanzania, Kigali
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 12 Septemba, 2024 ameungana na Majaji na Mahakimu kutoka Jumuiya ya Madola kutembelea Ikulu ya Mfalme Mutara III Rudahigwa na Makumbusho ya Rwesero, Nyanza nchini Rwanda ili kujionea utamaduni na maisha aliyokuwa anaishi wakati wa uhai wake.
Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya kuhitimisha Mkutano wa Kimataifa uliokuwa unafanyika jijini hapa, kuzungumzia haki mazingira. Wakati wa ziara hiyo, sehemu ya Majaji na Mahakimu waliokuwa wanahudhuria Mkutano huo wameshiriki kikamilifu.
Msafara wa mabasi makubwa nane uliobeba washiriki wa Mkutano huo uliondoka katika Ukumbi wa Kimataifa Kigali majira ya saa 2.30 asubuhi kuelekea katika Ikulu hiyo iliyopo umbali wa kilometa 100 kutoka jijini Kigali.
Wakiwa katika Ikulu hiyo, washiriki wa Mkutano huo walipokelewa na Meneja Isdor Ndikumana, ambaye aliwapa maelezo mafupi kuhusu eneo hilo na baadaye kutembezwa katika maeneo mbalimbali na Mwongoza Watalii, Bw. Virgile Shirirungu.
Majaji hao wamejionea makazi ya zamani ya Mfalme Rudahigwa yenye kuvutia na baadaye nyumba aliyokuwa anaishi kabla ya kuaga dunia mwaka 1959. Kadhalika, Majaji na Mahakimu hao walipata fursa ya kuona na kujifunza utamaduni na maisha ya Wafalme wa Rwanda, kuanzia Mfalme Yuhi Musinga na badaye mwanaye, Mfalme Rudahinga
Ule usemi kuwa mali zote ni za Mfalme ulijionesha wakati Bw. Shirirungu alipokuwa anaeleza maisha ya Mfalme Musinga wakati wa uhai wake. Alieleza kuwa kabla ya kuingia ukristu nchini Rwanda, Mfalme alikuwa na wake wengi na akihitaji mwanamke alikuwa anaenda kuchukua katika boma la mtu yoyote kadri yeye itakavyompendeza.
Alisema baada ya ukristo, Mfalme Rudahinga alikuwa na mke mmoja na aliishi naye kwa kipindi chote mpaka alipofariki. Baada ya kifo chake, mke wake alienda kuishi katika Mkoa wa Butare na alifikwa na mauti mwaka 1994 alipouawa wakati wa mauaji ya kimbali nchini Rwanda.
Baadaye msafara ulielekea katika Makumbusho ya Rwesero na kujionea vivutio mbalimbali. Makumbusho hayo yalikuwa ni makazi ya kisasa ya Mfalme Rudahinga yaliyoanza kujengwa mwaka 1957 na kukamilika mwaka uliofuatia, yaani 1958.
Hata hivyo, Mfalme Rudahinga hakufanimiwa kuishi kwenye jengo hilo jipya baada ya mwaka uliofuatia,yaani 1959 kufariki dunia. Kufuatia kifo hicho, Serikali ya Rwanda ikalitumia kwa shughuli za kiserikali kama Mahakama ya Upeo, Mahakama ya Rufani, Mahakama ya Biashara na Ofisini ya Mkurugenzi wa Mashtaka. Jengo hilo limekuwa Makumbusho ya Rwesero tangu tarehe 18 Mei, 2006.
Msafara umerejea katika Ukumbi wa Kimataifa Kigali majira ya saa 12.15 jioni, sawa na saa 1.15 usiku kwa Tanzania, hivyo kuhitimisha rasmi shughuli za Mkutano huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni