Jumatano, 2 Oktoba 2024

JAJI MWARIJA AFUNGUA MAFUNZO YA UHALIFU WA KIMTANDAO

Na MAGRETH KINABO NA INNOCENT KANSHA-Mahakama, Dares Salaam

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija, ambaye pia ni amidi wa Mahakama hiyo, amewataka wadau wa mnyororo wa Haki Jinai kutumia vyema fursa ya mafunzo yanayohusu makosa ya uhalifu kimtandao na ushahidi wa kielektroniki ili kupata maarifa na ujuzi utakawasaidia kutenda haki katika mashauri yanayohusu makosa hayo.

Mhe. Jaji Mwarija amesema hayo, leo tarehe 2 Oktoba, 2024 wakati akifungua mafunzo ya kujadili makosa ya uhalifu kimtandao, yanayofayika kwa muda wa siku tatu katika hoteli ya Four Points by Sheraton, iliyopo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

“ Nina washauri wadau wa myororo wa Haki Jinai kutumia nafasi hii ipasavyo kwa kujadiliana, kubadilishana uzoefu, maarifa, ujuzi na kuimarisha ushirikiano miongoni mwenu katika uendeshaji wa mashauri ya makosa ya uhalifu kimtandao na ushahidi wa kielektroniki ili kuwezesha haki kutendeka,” anasema Jaji Mwarija.

Mhe. Jaji Mwarija anafafanua kuwa mafunzo hayo yanayowalenga Majaji, Maafisa Mahakama na Maafisa Haki Jinai yana lengo la kuwaongezea ujuzi na maarifa ya kuyaendesha na kuyatolea maamuzi mashauri yanayohusiana na uhalifu wa kimtandao na mashauri mengine yanayohusisha ushahidi wa kielektroniki. 

Pia mafunzo hayo  yanatoa nafasi ya kujenga ufanisi kwa washiriki katika nyanja ya kisheria kwenye eneo la ushahidi wa kielektroniki na kutoa msaada wa pamoja wa kisheria, kwa kuwa  makosa ya uhalifu ya kimtandao yanahitaji ushirikiano wa kimataifa.

“Makosa ya uhalifu wa kimtandao ni changamoto ya kidunia inayotokana na maendeleo ya sayansi na tekinolojia ya karne ya 21, ni makosa yanayovuka mipaka ya kimataifa na kuathiri mtu mmoja  mmoja, uchumi na jitihada za Serikali za kukabiliana na makosa hayo. Hivyo mafunzo haya yatasaidia kuboresha  jitihada za pamoja za kukabiliana na uhalifu huo,”anasisitiza. 

Naye, Naibu Balozi wa Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Sally Hedley anasema Uingereza imetoa msaada wa paundi milioni 45 duniani  kwa ajili ya kupambana na uhalifu huo, na mafunzo hayo yameshatolewa kwa nchi za Caribbean, Afrika Magharibi, Kusini Mashariki mwa Asia na Ukanda wa Pacific.

Hedley anasema kwa mujibu wa ripoti ya Polisi wa Kimataifa inaonesha kwamba uhalifu huo wa kimtandao kwa nchi za Afrika umekuwa ukiongezeka kwa asilimia 25 mwaka hadi mwaka. 

“Ubalozi unaipongeza Tanzania kwa kuongeza juhudi na kuchukua hatua za kupunguza uhalifu wa kimtandao na kuwepo kwa maendeleo ya Mpango Mkakati wa Ulinzi dhidi ya Makosa ya Uhalifu wa Kimtandao kwa Ushirikiana wa Umoja wa Polisi Afrika wa Kupambana na Uhalifu wa Kimtandao(AFJOC).

Kwa upande wake, Mkuu wa Utawala wa Sheria wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, Dkt. Elizabeth Macharia anasema madhara ya uhalifu wa kimtandao duniani unatarajiwa kuongezeka thamani kutoka dola za Kimarekani trilioni 8.44 mwaka 2022 na inakadriwa kufikia takribani dola za kimarekani trilioni 23.84 ifikapo mwaka 2027, huku Bara la Afrika likipoteza dola za Kimarekani bilioni nne kwa mwaka kutokana na uhalifu huo, sawa na asilimia 10 ya Pato lake la ndani.

 

Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Dkt. Paul  Kihwelo amesema yameandaliwa na chuo hicho kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo wa Kimataifa wa Uingereza.

 

Mafunzo hayo yamehusisha Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar 15, Naibu Wasajili wanne, Mahakimu 12, Waendesha Mashtaka nane na Wapelelezi saba. Wawezeshaji wa mafunzo hayo wanatoka Tanzania na Uingereza, ambapo watajadiliana juu ya sheria ya uhalifu wa kimtandao na ushahidi wa kielektroniki.

 

Washiriki wa mafunzo hayo,Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka- Ilala, Ellen Masululi anasema mafunzo yatasaidia kuwepo kwa ushahidi unaojitosheleza ambao utasaidia uendeshaji wa mashauri mahakamani na kwao pia ni fursa ya kutoa ushauri. Wakati Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Iringa, Mhe.Honorious Kando, anaongeza kwamba mafunzo yatawasaidia kuwajengea uelewa mzuri wa makosa ya uhalifu wa kimtandao na sheria mpya ili kuiwezesha Mahakama kutenda haki.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija, ambaye pia ni amidi wa Mahakama hiyo akifungua mafunzo ya makosa ya uhalifu wa kimtandao na ushahidi wa kielektroniki leo tarehe 2 Oktoba, 2024. Mafunzo hayo yanayofayika kwa muda wa siku tatu katika hoteli ya Four Points by Sheraton, iliyopo jijini Dar es Salaam.


Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Dkt. Paul  Kihwelo akifafanua jambo wakati wa hafla ya kufungua mafunzo hayo.


Naibu Balozi wa Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Sally Hedley akitoa neno kwa washiriki wa mafunzo.

Mkuu wa Utawala wa Sheria wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, Dkt. Elizabeth Macharia akielezea umuhimu wa Mafunzo hayo.

Sehemu ya Wageni Mashuhuri wakimsikiliza Mkuu wa Utawala wa Sheria wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, Dkt. Elizabeth Macharia (hayupo pichani) akielezea umuhimu wa Mafunzo hayo.

Sehemu ya Washiriki wa Mafunzo hayo wakifuatilia jambo wakati wa hafla ya ufunguzi.

Sehemu ya Washiriki wa Mafunzo hayo wakifuatilia jambo wakati wa hafla ya ufunguzi.

Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao ni Washiriki wa Mafunzo hayo wakifuatilia jambo wakati wa hafla ya ufunguzi.

Sehemu ya Washiriki wa Mafunzo hayo wakifuatilia jambo wakati wa hafla ya ufunguzi.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wanaoshiriki mafunzo hayo.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wakufunzi wa mafunzo hayo.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wanaoshiriki mafunzo hayo.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wanaoshiriki mafunzo hayo.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Sekretarieti ya mafunzo hayo.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wapelelezi na waendesha mashitaka  wa Serikali wanaoshiriki mafunzo hayo.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wananchama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wanaoshiriki mafunzo hayo.

(Picha na Innocent Kansha- Mahakama)























































































































Hakuna maoni:

Chapisha Maoni