Jumatano, 2 Oktoba 2024

KILA MDAU ATEKELEZE WAJIBU WAKE IPASAVYO - JAJI MUGETA

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta ametoa rai kwa kila mdau wa Mahakama katika Kanda hiyo kuhakikisha anatimiza wajibu wake na kuepuka kuwa kikwazo cha kukwamisha Mahakama kumaliza mashauri kwa wakati.

Akizungumza jana tarehe 01 Oktoba, 2024 kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha katika kikao cha kusukuma mashauri na kuweka mikakati mbalimbali kuhakikisha mashauri yanasikilizwa kwa wakati, Mhe. Mugeta alisema vikwazo vya mara kwa mara husababisha kuwanyima wananchi kupata haki zao kwa wakati.

“Wadau wote wa mashauri waache uvivu katika kutimiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kuandaa mashahidi mapema iwezekanavyo ili mashauri yamalizike kwa wakati na kuepuka kutengeneza mashauri ya mlundikano bila sababu za msingi,” alisema Mhe. Mugeta.

Jaji Mugeta aliwashukuru wajumbe kwa kuitika wito wa kuhudhuria kikao hicho na kuongeza kuwa, ni muhimu wadau kukutana na kutathmini mwenedo wa ufanyaji kazi katika kuhakikisha Mahakama inapokea na kusikiliza mashauri kwa wakati. 

Katika kikao hicho, mashauri ya mlundikano yalijadiliwa na kuwekewa mkakati wa kuyamaliza ikiwa ni pamoja na Mahakama Kuu Arusha kufanya vikao maalum vya kusikiliza mashauri (sessions), kila mdau kutimiza wajibu wake katika shauri, kukamilisha upelelezi kwa wakati na ushirikiano baina ya wadau.

Kwa upande wake Mwendesha Mashtaka Mfawidhi wa Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Arusha, Bw. Abdalla Chavula ameahidi kuwa, atahakikisha upande wa Jamhuri unakamilisha taratibu zake kwa wakati ikiwa ni pamoja kukamilisha upelelezi kwa wakati na kuandaa mashahidi mapema ili mashauri yachukue muda mfupi mahakamani.

Katika kuhakikisha kuwa, Mahakama Kanda ya Arusha inamaliza mwaka huu bila mashauri ya mlundikano, tayari imeandaa na kuanza kutekeleza mkakati wa kumaliza mashauri ya mlundikano kwa kufanya kikao cha kusikiliza mashauri (session) mwezi Septemba 2024 na vikao hivyo vinaendelea kufanyika mwezi huu.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe kutoka Taasisi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Ofisi ya upelelezi Mkoa wa Arusha, Ofisi ya Mganga Mkuu Hospitali ya Mkoa ‘Mount’ Meru, Gereza la Mkoa Arusha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Arusha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta akisisitiza jambo wakati wa Kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika jana tarehe 01 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Sehemu ya wajumbe walioshiriki Kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika jana tarehe 01 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Mkaguzi Msaidizi wa Magereza Mkoa wa Arusha, Bw. Pius Masonda akichangia jambo wakati wa Kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika jana tarehe 01 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Mhe. Aisha Ndossy (kushoto) na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Mhe. Sheila Manento ( kulia) wakisikiliza kwa makini kilichokuwa kikijadiliwa wakati wa Kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika jana tarehe 01 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni