Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Lushoto
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mahakimu 88 wapya kuzingatia maadili
wanapotekeleza majukumu yao na kubadili fikra na mitazamo katika huduma za
Mahakama.
Mhe. Prof. Juma alitoa
wito huo jana tarehe 30 Novemba, 2024 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto baada ya kuwaapisha Mahakimu hayo na kisha kufungua mafunzo elekezi ambayo
yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo hicho.
“Kubadili fikra na
mitazamo sio kazi nyepesi na asilimia kubwa ya kazi ya Hakimu ni uadilifu. Unaweza
kuwa na akili nyingi sana kupindukia, lakini ukazitumia zile akili kupindisha
haki kwa sababu huna maadili,” alisema katika hafla hiyo iliyohuduriwa na
Viongozi mbalimbali wa Mahakama.
Jaji Mkuu alibainisha
kuwa kazi kubwa iliyofanywa na Mahakama ya Tanzania kama sehemu muhimu ya
mageuzi na maboresho ya huduma za Mahakama ni kubadili fikra na kuondoa
tamaduni na kawaida zilizozoeleka ambazo zilikuwa zikiathiri ufanisi, uwazi,
weledi na uharaka wa utoaji huduma.
Alieleza kuwa fikra chanya
inayosukuma maboresho na mabadiliko ni kutoa huduma bora zinazomlenga na
kumjali mwananchi, kumfikishia huduma kwa wakati.
Mhe. Prof. Juma alibainisha
pia kuwa kila baada ya takriban miaka mitatu, Mahakama imekuwa ikifanya
tathmini ya maboresho, kutaka kujua ni kwa kiasi gani, maboresho yameleta
huduma zinazowaridhisha watumiaji wa huduma za Mahakama.
“Kuweni tayari utendaji
wenu kupimwa na mifumo ya teknolojia, kuweni tayari kupimwa kupitia maoni na
mapendekezo
ya wananchi kupitia programu za mrejesho na kituo cha huduma kwa mteja,”
alisema.
Jaji Mkuu aliwahimiza
Mahakimu hao kusoma kwa makini, ripoti ya utafiti iliyotayarishwa na Taasisi
isiyo ya Kiserikali iitwayo Repoa, kuhusu kuridhika kwa watumiaji wa huduma za Mahakama
2023.
Alieleza kuwa ripoti ya
2023 ililenga kutoa mrejesho kwa Mahakama kuhusu huduma zake inazozitoa
ikilinganishwa na matarajio ya watumiaji na watumishi tangu utafiti wa awali
ulipofanyika mwaka 2015, 2019 hadi 2023.
“Ripoti ya Repoa
iliwasilisha tathmini ya watumiaji kuhusu ubora wa huduma za Mahakama kwa
kulinganisha ubora ulivyokuwa mwaka 2019 na 2023. Wajibu wenu Mahakimu wapya ni
kuhakikisha viwango havishuki wakati Repoa watakapofanya utafiti ujao,”
alisema.
Kwa mujibu wa utafiti huo,
kuhusu hudma za Mahakama za Mwanzo kwa mwaka 2019, asilimia 57 ya wananchi
walisema ni nzuri, asilimia 36 walisema wastani na asilimia sita walisema huduma
ni mbaya, lakini mwaka 2023, asilimia 64 walisema huduma za Mahakama za Mwanzo
ni nzuri, asilimia 31 walisema wastani na asilimia nne walisema huduma ni mbaya.
Kwa upande wa Mahakama za
Wilaya, kwa mwaka 2019, wananchi asilimia 55 walisema huduma ni nzuri, wastani
ilikuwa asilimia 37 na huduma mbaya ni asilimia saba, lakini mwaka 2023,
utatifi unaonesha asilimia 62 ya wananchi walisema huduma zinazotolewa ni
nzuri, wastani ilikuwa asilimia 33 na mbaya ilikuwa asilimia tatu.
Kuhusu Mahakama za Hakimu
Mkazi, utafiti unaonesha asilimia ya wananchi waliosema huduma zinazotolewa ni
nzuri ni asilimia 54, waliosema huduma ni za wastani ni asilimia 36 na
waliosema huduma ni mbaya ni asilimia tisa kwa mwaka 2019, lakini kwa mwaka
2023, waliosema huduma nzuri walikuwa asilimia 62, wastani asilimia 33 na mbaya
asilimia tatu.
Kwa upande wa Mahakama
Kuu, utafiti unaonesha asilimia ya wananchi waliosema huduma ni nzuri ni asilimia
53 kwa mwaka 2019, waliosema huduma ni za wastani ni asilimia 40 na waliosema
huduma ni mbaya ni asilimia tatu, lakini kwa mwaka 2023, waliosema huduma nzuri
walikuwa asilimia 62, wastani asilimia 35 na mbaya asilimia mbili.
Aidha, kwa upande wa
Mahakama ya Rufani, kwa mwaka 2019, asilimia ya wananchi waliosema huduma ni
nzuri ni asilimia 82, waliosema huduma ni za wastani ni asilimia tisa na
waliosema huduma ni mbaya ni asilimia tisa, lakini kwa mwaka 2023, waliosema
huduma nzuri walikuwa asilimia 75, wastani asilimia 25 na mbaya asilimia nne.
Viongozi wa Mahakama ya
Tanzania waliohudhuria hafla ya uapisho na ufunguzi wa semina hiyo elekezi kwa
Mahakimu 88 wapya ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la
Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Mary Levira na Jaji
wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe.
Dkt. Paul Kihwelo.
Wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Revocati Mteule, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sundi Fimbo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni