• Asisitiza uadilifu, weledi na uwajibikaji kwa watumishi
Na LUSAKO MWANG’ONDA, Mahakama-Iringa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Dunstan Beda Ndunguru amezindua jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Mahenge na kuwataka watumishi wa Mahakama hiyo kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji katika kuwatumikia wananchi.
Jengo hilo la Mahakama ya Mwanzo Mahenge limejengwa katika Kata ya Mahenge wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo hilo jana tarehe 30 Novemba, 2024, Mhe. Ndunguru amesema, “leo hii tunazindua jengo hili la Mahakama, ni jengo zuri na linaipa heshima Mahakama yetu, uzuri wa hili jengo hautakuwa na maana kama watumishi wa Mahakama hii hatutafanya kazi kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji katika kuwatumikia wananchi.”
Jaji Ndunguru alisema ni vema watumishi wa Mahakama kufahamu kuwa, wananchi wana imani kubwa na chombo hicho kwa kuwa ndicho kilichokasimiwa jukumu la utoaji haki, hivyo ni budi kwa kila mtumishi kuwa na uadilifu usiotia mashaka ili imani ya wananchi kwa Mahakama iendelee.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilolo, Bw. Stomen Kyando ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, aliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kujenga jengo hilo katika eneo hilo. “Tunaishukuru sana Mahakama ya Tanzania kwa kujenga Mahakama hii nzuri, ambayo inakwenda kuwasaidia Watanzania na hasa wa hizi kata nne za Tarafa ya Mahenge,” alisema Bw. Kyando.
Bw. Kyando alimuhakikishia Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kuwa, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama ili kuhakikisha kuwa inatekeleza majukumu yake ya utoaji haki pasipo na shida yoyote.
Aliongeza kuwa, ofisi yake haijapokea malalamiko yoyote yanayotokana na huduma ya Mahakama na kwamba hiyo yaweza kuwa ishara kuwa Mahakama inafanya kazi vizuri.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Melea Richard Mkongwa akizungumza wakati akitoa taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa Mahakama hiyo, aliishukuru Mahakama ya Tanzania pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kufanikisha ujenzi wa Mahakama hiyo.
Aliwataka wananchi waliofurika katika hafla hiyo ya uzinduzi kulitunza jengo hilo ambapo alisema, “hili jengo tunalikabidhi kwenu likiwa linapendeza na nyie ndo watumiaji wakubwa wa jengo hili, hivyo ninawaomba sana kuendelea kulitunza jengo hili ili kusitokee uharibifu wa namna yoyote hapa.”
Hafla ya uzinduzi wa jengo hilo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Mahakama, Vyama vya Siasa na Viongozi wa Dini, wananchi kutoka Kata mbalimbali zinazounda Tarafa ya Mahenge waliojitokeza kwa idadi kubwa katika hafla hiyo.
Muonekano wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Mahenge lililozinduliwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Beda Ndunguru akizungumza na mamia ya watu waliohudhurua hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Mahenge (hawapo katika picha).
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Melea Richard Mkongwa akisoma taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Mahenge.
Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa wakiimba ushairi katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Beda Ndungura (katikati) akiwa katika picha ya pamoja Viongozi mbalimbali pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu Iringa waliohudhuria hafla hiyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Beda Ndunguru akipanda mti mbele ya jengo la Mahakama ya Mwanzo Mahenge kuashiria ufunguzi rasmi wa jengo hilo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilolo, Bw. Stomen Kyando (kulia) akipanda mti mbele ya jengo hilo kuashiria ufunguzi rasmi wa jengo hilo.
Sehemu ya wananchi wa Mahenge waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Mahenge.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni