• Abainisha kuhusu hatua za maandalizi zilipofikia kuelekea Mkutano Mkuu wa 21 wa EAMJA
Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara na Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), Mhe. John Rugalema Kahyoza amesema kuwa nchi wanachama wa Chama wa Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) zinanufaika kutokana na Chama hicho kujikita katika kukuza, kuimarisha misingi inayosaidia kujenga ufanisi katika usimamizi wa haki, utawala wa sheria, Utawala Bora na Uhuru wa Mahakama.
Mhe. Kahyoza ameyasema hayo leo tarehe 01 Desemba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) utakaofanyika kuanzia tarehe 02 hadi 07 Desemba, 2024 katika Hoteli ya Gran Melia’ jijini Arusha.
Aidha, Mhe. Kahyoza amezungumzia kwa upana kuhusu malengo ya Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) kuwa ni pamoja na kukuza na kulinda Haki za Binadamu.
“Malengo mengine ni kukuza na kuelewa kazi za kimahakama kupitia tafiti, ubadilishanaji wa taarifa, mafunzo kwa watumishi, kujenga mahusiano ya kikazi na kubadilisha uzoefu na mawazo kati ya nchi wanachama wa EAMJA,” amesema Jaji Kahyoza.
Kadhalika, ameongeza kuwa, Chama cha EAMJA kilianzishwa kwa malengo ya kujenga udugu, kubadilishana uzoefu na kuweka utengamano wa ksheria baina ya nchi wanachama ikiwa ni sehemu ya kuwezesha wananchi kuweza kufanya mahusiano husuani ya kibiashara katika mazingira wezeshi kisheria na kijamii.
Akizungumzia maandalizi ya Mkutano huo, Mhe. Kahyoza amewaeleza Wanahabari kuwa, maandalizi yamefikia hatua nzuri na tayari wameanza kupokea wageni tangu jana na zoezi la kupokea wageni linaendelea.
“Kuwepo kwa kikao hiki leo ni kimelenga kuufahamisha umma juu ya uwepo wa mkutano huu na na kuwajuza kuwa tunaendelea vizuri na maandalizi ya Mkutano,” amesema Mhe. Kahyoza.
Amezitaja nchi ambazo zitakazoshiriki katika mkutano huo kuwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Zanzibar, Burundi na Sudani ya Kusini na kuongeza kuwa mwaka huu muitikio wa ushiriki wa Mkutano kutoka kwa wajumbe ni mkubwa.
Kaulimbiu ya Mkutano huo ambao unatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 03 Desemba, 2024 inasema ‘Uboreshaji wa Mifumo ya Utoaji Haki kwa ajili ya kujenga na kuimarisha utengamano na ukuzaji wa uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.’
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni