Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa
Chama cha Majaji na Mahakimu kutoka Nchi za Afrika Mashariki unaofanyika jijini
Arusha, kuwaleta pamoja zaidi ya washiriki 300 kutoka Ukanda huo, umeanza leo
tarehe 2 Desemba, 2024.
Mapema asubuhi
kimefanyika kikao cha Baraza Tendaji la Chama cha Majaji na Mahakimu wa Afrika
Mashariki kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji, changamoto na mafanikio
lukuki ambayo tayari yameshapatikana.
Kikao pia kimetoa taswira
halisi kuhusu ushiriki wa wanachama kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka na mambo
mbalimbali yatakayofanyika kwa kipindi cha takribani siku tano.
Mada mbalimbali
zitajadiliwa wakati wa Mkutano, ikiwemo Kuimarisha Msingi wa Mahakama: Mahakama
kama Msingi wa Mnyororo wa Haki Jinai, Maboresho katika Kuimarisha Utoaji wa
Haki; Uoanishaji Sheria za Kazi Afrika Mashariki ili Kuboresha Utatuzi wa
Migogoro; Wajibu wa Mifumo ya Kielektroniki ya Usimamizi wa Mashauri katika
Kuboresha Ufanisi wa Mahakama na Uamuzi wa Makosa Yasiyo na Mipaka katika
Mahakama za Afrika Mashariki: Mfumo na Changamoto za Kisheria.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri,
Bi. Suzanne Ndomba ni miongoni mwa Wataalamu wa Sheria watakaochokoza mada
kwenye Mkutano huo, huku Mhadhiri Nguli wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na Shule ya Sheria kwa Videndo, Prof. Hamudi Ismail Majamba akiwa mmoja
wa waongoza Majopo kujadili mada hizo.
Watanzania wengine
watakaoshiriki kwenye Majopo kujadili mada hizo ni Jaji wa Mahkama Kuu
Zanzibar, Mhe. Khadija Shamte Mzee, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Aisha Sinde na Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri, Mhe. Desdery Kamugisha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni