Jumatatu, 27 Januari 2025

ENDELEENI KUUNGA MKONO MABORESHO NDANI YA MAHAKAMA; PROF. OLE GABRIEL

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ametoa rai kwa Watumishi wa Mahakama nchini kuendelea kuwa sehemu ya maboresho yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama ya Tanzania.

Prof. Ole Gabriel ameyasema hayo leo tarehe 27 Januari, 2025 alipotembelea mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.

“Rai yangu kwa watumishi wa Mahakama ni kwamba wanatakiwa kuendelea kuwa sehemu ya maboresho ya Taasisi ikiwa ni pamoja na kuunga mkono matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuwa ni sehemu muhimu ya maboresho,” amesema Mtendaji Mkuu.

Akizungumzia kuhusu Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria ya mwaka huu “Tanzania ya 2050: Nafasi Ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika kufikia malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo,” Prof. Ole Gabriel amesema kuwa, anatarajia kuiona Mahakama mwaka 2050 kuwa ya kifanisi zaidi.

“Ni matarajio yangu kuwa, Mahakama ya 2050 itaendelea kuwa kinara kwa ufanisi, itaendelea kuwa juu zaidi katika ngazi za kimataifa,” ameeleza.

Kadhalika, amesema kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa kushikamana/ushirikiano wa karibu na Mihimili ya Serikali pamoja na Bunge ili kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Ameongeza kuwa, utawala bora bila haki  ni kazi hivyo Taasisi za Haki madai ni muhimu sana.

Kadhalika, Mtendaji Mkuu amemshukuru Mgeni Rasmi aliyefungua Wiki ya Sheria, Rais Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kukubali kuungana na Mahakama kuzindua Wiki hiyo muhimu kwa umma na kwamba anathamini mchango wake kama mwanzilishi wa maboresho ya Mahakama.

Akiwa katika mabanda hayo, Mtendaji Mkuu amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na watu wenye mahitaji maalum waliofika katika Maonesho ya Wiki ya Sheria kupata elimu kuhusu Mahakama na Sheria kwa ujumla.

Mabanda aliyotembelea Mtendaji Mkuu ni ya Mahakama ya Tanzania,  Kituo cha Huduma kwa Mteja (Call Centre), Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tume ya Kurekebisha Sheria, TAKUKURU, Wizara ya Katiba na Sheria, Mkemia Mkuu wa Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Viwanja vya Nyerere 'Square' kutembelea mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Sheria leo tarehe 27 Januari, 2025.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisalimiana na watu wenye mahitaji maalum waliofika leo tarehe 27 Januari, 2025 katika Viwanja vya Nyerere 'Square' kupata huduma ya elimu ya taratibu za Mahakama na Sheria kwa ujumla.

Picha mbalimbali zikimuonesha Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akipata maelezo kutoka kwenye sehemu ya mabanda mbalimbali yaliyopo kwenye Maonesho ya Wiki ya Sheria. Mtendaji Mkuu ametembelea mabanda hayo Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma leo tarehe 27 Januari, 2025.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni