Na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama-Dodoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo leo tarehe 27 Januari, 2025 ametembelea mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Sheria yanaoyafanyika katika viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma ili kujionea shughuli mbalimbali ambazo zinaendelea katika maonesho hayo.
Mhe. Dkt. Masabo aliwasili katika viwanja hivyo majira ya saa 4 Asubuhi na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama kisha kutembelea mabanda mbalimbali.
Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kutembelea mabanda hayo Mhe. Dkt. Masabo amesema, “nianze kwa kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maoni yangu maonesho ya mwaka huu yamefana ukilinganisha nay a miaka iliyopita.”
Kadhalika, Jaji Mfawidhi huyo amezungumzia kuhusu Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria ya mwaka huu isemayo; “Tanzania ya 2050: Nafasi Ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika kufikia malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo,” amesema kuwa, Mahakama kama Mhimili ambao kikatiba umepewa jukumu la utoaji haki, inayo nafasi kubwa ya kuhakikisha kwamba Dira ya Taifa ya 2050 inafikika kwa mafanikio makubwa katika maendeleo.
Ameongeza kuwa, ni vema vyombo vyote na Taasisi za usimamizi wa haki na sio tu haki madai lakini pia jinai kuhakikisha kwamba wanashirikiana kutoa haki na kuhakikisha kuwa Nchi yetu inapiga hatua kubwa katika maendeleo.
“Sisi kama Taasisi kama Mhimili ambao kikatiba ndo umepewa jukumu la utoaji haki tunaona kwamba tunayo nafasi kubwa sana ya kuweza kuhakikisha kwamba tunaifikia Tanzania ya 2050 kwa mafanikio makubwa sana katika maendeleo,” amesema Mhe. Dkt. Masabo.
Kadhalika, Jaji Mfawidhi amezungumzia Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambapo amewapongeza kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wamekuwa wakifanya katika maeneo ambayo wanayafanyia kazi kwa maana ya kwamba utoaji elimu kwa wananchi kuhusiana na haki za Wanawake na za Watoto wa kike na wa kiume, kujenga uwezo wanachama wao ambao ni Majaji na Mahakimu wanawake.
“Kwakweli ni kazi kubwa ambayo TAWJA wamekuwa wakiifanya kwa miaka 25 sasa tangu imeanzishwa na imekuwa na matunda makubwa sana katika utendaji kazi wetu sisi Mahakimu na Majaji lakini pia katika jamii katika kutetea haki za wanawake pamoja na watoto” amesema Mhe.Dtk.Masabo
Vilevile ametoa rai kwa Chama hicho kuendelea kufanya kazi zao zaidi ya zile ambazo wamefanya katika miaka 25 iliyopita, tumejipanga kama TAWJA na kuhakikisha kwamba tunapofikisha miaka hamsini kama ambavyo kauli mbiu yetu inavyosema
Ameongeza kwa kushukuru na kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa nafasi kwa wanawake ndani ya Mahakama tofauti na zamani ambapo fani ya sheria ilionekana kama ni kazi ya kiume zaidi.
Baadhi ya mabanda ambayo Jaji Masabo ametembelea katika Maonesho ya Wiki ya Sheria ni pamoja na; Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mamlaka ya Kuthibiti Madawa ya Kulevya (DCEA), Jeshi la Polisi, Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Banda la TAWJA.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (wa pili kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali alipotembelea banda hilo lililopo katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni