Jumatatu, 27 Januari 2025

MAHAKAMA, WADAU KUTOA ELIMU YA SHERIA BURE RUVUMA

 Na NOEL SYLIVESTER-Mahakama, Songea

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abas Ahmed amewahimiza Wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Sheria ili kupata elimu ya sheria kwenye masuala mbalimbali.

Mhe. Ahmed alitoa rai hiyo kwenye uzinduzi wa maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vy Soko Kuu Songea.

Mkuu wa Mkoa alibainisha kuwa Wananchi wengi wanauhitaji na changamoto ya kujua sheria mbalimbali, kama za ndoa, ardhi, mirathi, hivyo ni vema wakajitokeza katika maadhimisho hayo kwani elimu ya sheria itakayotolewa na Mahakama na Wadau itakuwa bure.

Aliongeza kuwa kwa mwaka 2025 Mahakama kwa kushirikiana na Wadau watatembelea maeneo mbalimbali na kutoa elimu  bure na msaada wa kisheria kwa Wananchi katika  Shule za Sekondari na Msingi, Mabaraza ya Usuluhishi, Mabaraza ya Ndoa,  Sokoni, mikutano ya hadhara na katika radio.

“Ninatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kutumia Wiki ya Sheria kujitokeza kwa wingi kujua sheria mbalimbali za ndoa, ardhi na kupata msaada wa kisheria bure,”alisema.

Awali akitoa taarifa ya maadhimisho hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe.James Karayemaha alisema kuwa Wiki ya Sheria inalenga kutoa elimu ya sheria kwa wananchi kwa kuwafuata katika maeneo mbalimbali kama mikutano ya hadhara, katika Taasisi za umma kama shule, vijiwe vya bodaboda, mama ntilie pamoja na wahudumu wa bar.

Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Wiki na Siku ya Shweria inasema, “Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazozimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Songea, Mhe James Karayemaha akisalimia Wananchi kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria mkoani Ruvuma.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abas Ahmed akizungumza kwenye uzinduzi huo.

Jaji wa Mahakama Kuu Songea, Mhe Emmanuel Kawishe(katikati).

Jaji Mfawidhi akiwa na Mkuu wa Mkoa pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Songea wakishiriki matembezi kuelekea Viwanja vya Soko Kuu Songea.

Matembezi kuelekea Soko Kuu Songea.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni