Jumatatu, 27 Januari 2025

MWITIKIO WA KIHISTORIA UZINDUZI WIKI YA SHERIA MOROGORO

Na EVELINA ODEMBA – Mahakama, Morogoro

Maelfu ya Wananchi wamejitokeza kushuhudia uzinduzi wa Wiki ya Sheria ambao kwa Kanda ya Morogoro ulifanyika kwenye Viwanja vya Stendi ya Daladala ya zamani iliyoko Morogoro Mjini.

Uzinduzi huo ulihudhuliwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Kilakala, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi alisema kuwa amefarijika kwa uwepo wa Maadhimishi ya Wiki ya Sheria na kutoa rai kuwa suala la unyanyasaji wa kijinsia lipewe kipaumbele kikubwa wakati wa zoezi la utoaji elimu.

“Nimefurahi kusikia kuwa wakati wa Wiki ya Sheria Wananchi watapewa elimu juu ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, masuala haya yamekuwa ni tatizo kubwa sana kwa Mkoa wa Morogoro,” alisema.

 Aliwaomba Wananchi wa Mkoa huo kuitumia vyema fursa hiyo kufika kwenye mabanda ili kupata uelewa juu ya masuala hayo na mengine mengi yanayohusu sheria.

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Latifa Mansoor, ambaye alihudhuria ufunguzi huo alisema kuwa katika Wiki ya Sheria mkoani Morogoro wamejipanga kuwafikia Wananchi mbalimbali.

Alitoa wito kwa wote ambao wamekuwa na shida mbalimbli za masuala ya kisheria na hawafahamu namna ya kuifikia Mahakama wafike katika mabanda ili waweze kutatuliwa shida zao na kupatiwa elimu.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga alipalilia suala la Wananchi kuitumia vyema nafasi ya Wiki ya Sheria kwa kuwa wakati mwingine wanapata changamoto ya kuwafikia wanasheria ili kupata ushauri wa masuala yanayohusu sheria.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala (wa tatu kulia), akifuatiwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Latifa Mansoor wakiongoza Wananchi kwenye matembezi maalumu ya shamla shamla za uzinduzi wa Wiki ya Sheria.




Matukio katika picha wakati wa maandamano (juu na chini).


Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala akizunguza wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Sheria mkoani Morogoro.

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Latifa Mansoor akizungumza wakati wa uzinduzi huo.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria.

Watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro (juu na chini) wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi huo.


Burudani ya ngoma za asili ikiendela katika shamla shamla za uzinduzi wa Wiki ya Sheria Kanda ya Morogoro.

Matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni