Alhamisi, 23 Januari 2025

MAHAKIMU KIGOMA WAPIGWA MSASA USIKILIZAJI MASHAURI YA UCHAGUZI

Na AIDAN ROBERT-Mahakama, Kigoma

Mahakama Kanda ya Kigoma hivi karibuni iliendesha mafunzo kwa Mahakimu wa Mahakama za Wilaya ili kuwawezesha kusikiliza mashauri yanayotokana na uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka 2024.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi alifungua mafunzo hayo kwa njia ya mtandao na kuwasisitiza Mahakimu hao kuzingatia yale yote watakayofundishwa na wawezeshaji.

“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu katika jamii, hivyo ni vyema Mahakimu kujipanga vizuri na kufanya kazi kwa ufanisi ili kuwezesha mashauri kumalizika kwa wakati,” alisema. 

Aidha, aliwahimiza Mahakimu hao kuzingatia na kutumia Katiba, Sheria na miongozo mingine mbalimbali, ikiwemo hukumu za Mahakama kama nyenzo muhimu wakati wa usikilizaji wa  mashauri hayo.

Akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo kwa njia ya mtandao, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Dkt. Emmanuel Kawishe aliwaeleza Mahakimu hao kutambua kuwa mashauri yanayohusu uchaguzi yanamsukumo mkubwa wa kisiasa, hivyo ni vyema kujishibisha maarifa ya kitaaluma yatakayowasaidia kutenda haki bila upendeleo.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora Mhe. Pamela Mazengo, ambaye alikuwa mtoa mada aliyowasilisha kwa njia ya mtandao, aliwasihi Mahakimu hao kuzingatia taratibu zote za uendeshaji wa mashauri ya madai ili kuondoa mwanya kwa wenye mashauri kudhani haki haiwezi kutendeka.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa alisema kuwa Mahakimu wa Mahakama za Wilaya ni Viongozi muhimu katika Mahakama zao, hivyo wanatakiwa kulinda maadili yao na taswila ya Mahakama kwa ujumla.

Mahakimu walioshiriki katika mafunzo hayo wametoka katika Mahakama za Wilaya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Uvinza, Buhigwe na Kakonko.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi (katikati) akiwa katika picha na Mahakimu wa Wilaya waliopewa dhamana ya kusikiliza mashauri ya uchaguzi katika Mkoa wa Kigoma mara baada ya kufungua mafunzo hayo kwa njia ya mtandao huku akiwa katika ofisi yake Mahakama Kuu Kigoma na washiriki wakiwa Mahakama ya Wilaya Kasulu.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe.  Dkt. Emmanuel Kawishe akitoa mada kwenye mafunzo hayo kwa njia ya mtandao.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo, akiwa anatoa mada katika mafunzo hayo kwa njia ya mtandao.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, (aliyesimama) akitoa mada.

Picha ya pamoja ya  Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Fadhili Mbelwa (katikati) na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibondo, Mhe. Maila Makonya, kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu, Mhe. Iman Batenzi na waliosimama nyuma ni Mahakimu toka Wilaya ya Kigoma, Uvinza, Buhigwe na Kakonko.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni