• Ampongeza Jaji Mkuu kwa usimamizi mzuri wa matumizi ya TEHAMA mahakamani
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 22 Januari, 2025 amewaapisha Majaji wanne wapya wa Mahakama ya Rufani katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Majaji hao pamoja na Viongozi wengine, Mhe. Dkt. Samia amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kusimamia vema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mahakamani.
“Nawapongeza Majaji niliowaapisha kwa uteuzi katika Mahakama ya Rufani lakini pia napenda kukupongeza Jaji Mkuu kwa kuendelea vyema katika matumizi ya TEHAMA,” amesema Mhe. Dkt. Samia.
Aidha, Rais Samia amewakumbusha Viongozi na Watumishi wa Mahakama kuendelea kutumia vema uhuru walionao kwa kutekeleza ipasavyo majukumu yao kwa kuzingatia kanuni za utoaji wa haki.
Kadhalika, Mhe. Dkt. Samia ametoa rai kwa Viongozi wengine aliowaapisha kufanya kazi vizuri na kusimamia wajibu wao mahali walipo ili matunda yaonekane.
Akitoa salaam katika hafla hiyo, naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Rais Samia kwa kuongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na kusema kuwa imeongeza idadi kutoka Majaji 35 hadi 39.
“Napenda kuchukua nafasi hii kushukuru kwa ongezeko la Majaji kabla ya uteuzi wa Majaji hawa kulikuwa na jumla ya Majaji 35 wa Mahakama ya Rufani, ongezeko la Majaji hawa kunaongeza idadi kuwa 39,” amesema Mhe. Prof. Juma.
Jaji Mkuu ameongeza kuwa, ongezeko la Majaji hao linaongeza pia idadi ya majopo kutoka 11 hadi majopo 12, ambapo amesema, “ongezeko la Majaji litasaidia pia kupunguza mlundikano wa mashauri sambamba na kupunguza msongamano wa mahabusu gerezani.”
Majaji walioapishwa leo ni Mhe. Mhe. Latifa Alhinai Mansoor, Mhe. Jaji George Mcheche Masaju, Mhe. Dkt. Deo John Nangela na Mhe. Prof. Ubena John Agatho.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya na wengine.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Latifa Alhinai Mansoor kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwenye hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 22 Januari, 2025.
Mhe. Latifa Alhinai Mansoor akila kiapo cha kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Mhe. George Mcheche Masaju akiapa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Mhe. Dkt. Deo John Nangela akila kiapo kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe.Prof. Ubena John Agatho kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwenye hafla iliyofanyika leo tarehe 22 Januari, 2025 Ikulu Chamwino jijini Dodoma.
Viongozi wa Mahakama waliohudhuria hafla ya uapisho wa Majaji wanne wa Mahakama ya Rufani na Viongozi wengine wa Serikali iliyofanyika leo tarehe 22 Januari, 2025 Ikulu Chamwino jijini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye hafla ya kuwaapisha Majaji wa Mahakama ya Rufani, Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Januari, 2025.
(Picha na IKULU)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni