Jumanne, 28 Januari 2025

SHANGWE ZATAWALA MAADHIMISHO YA WIKI YA SHERIA KANDA YA MOROGORO

Na EVELINA ODEMBA – Mahakama, Morogoro

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yamezinduliwa kwa shamla shamla katika Wilaya mbalimbali ambazo zipo chini ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mororogo, huku Wananchi wakijitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi uliofanyika tarehe 25 Januari, 2025.

Akizungumza wakati wa uzinduzi Morogoro mjini, Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye aliwahi kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor alisema kuwa Mahakama katika Wilaya zote itaitumia Wiki ya Sheria kutoa elimu na misaada ya kisheria bure kwa Wananchi.

“Hakuna haja ya Mwananchi kutumia gharama kusafiri toka Malinyi kuja mjini Morogoro kupata huduma ya msaada wa kisheria, napenda kuwahakikishia huduma hii itamfuata huko huko Malinyi na kwingineko ndani ya Kanda ya Morogoro,” alisema na kuongeza kuwa Mahakama Kanda ya Morogoro imejipanga vyema na wana wataalamu wa kutosha ambao watatoa huduma za kisheria na elimu bila malipo yeyote.

Kwa upande wa Wilaya ya MVOMERO, Wiki ya Sheria ilizinduliwa kwa kufanya matembezi ambayo yaliyoongozwa naMkuu wa Wilaya, Mhe. Judith Nguli. Mhe. Nguli alitoa wito kwa Wananchi kuhudhuria kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya utoaji elimu ili kujifunza mambo mbalimbali ya kisheria.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mvomero, Mhe. Anthony Ngowi alieleza kuwa miongoni mwa mada watakazoelimisha jamii ni pamoja na masuala ya mirathi, ndoa, malalamiko, dhamana na kero zote za jamii kisheria.

Nako wilayani MALINYI, Mkuu wa Wilaya, Mhe. Sebastian Waryuba aliwahimiza Wananchi kuitumia fursa hiyo adimu ya kupata elimu ya masuala ya sheria bure badala ya kusubiria mtu akiwa na kesi mahakamani ndipo anatafuta elimu ili kujua mchakato wa haki unavyokuwa.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Malinyi Mhe. Josiah Obasi alisema kuwa Mahakama wilayani humo imekusudia kutoa elimu kuendana na kauli mbiu kwa kushirikiana na Wadau wa Haki na elimu hiyo itatolewa maeneo mbalimbali ikiwemo shuleni, sokoni, vyuoni na kwenye Mabaraza ya Kata.

Katika Wilaya ya ULANGA, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bi. Saida Mahungu aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kutambua umuhimu wa elimu ya msingi ya sheria na kuanzisha Wiki ya Sheria nchini. Aliongeza kuwa maadhimisho hayo ni muhimu kwa kuwa yanawafikia Wananchi wa hali zote.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ulanga, Mhe. Christopher Bwakila alisema kuwa milango ya Mahakama ipo wazi kuwapokea Wananchi wenye changamoto mbalimbali za kisheria na wale wanaohitaji ufafanuzi wa masuala ya kisheriaa pia wanakaribishwa.

Huko wilayani KILOMBERO, uzinduzi ulianza kwa matembezi maalumu yaliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya, Mhe. Dustan Kyobya na baadaye kutaja maeneo yatakayotolewa elimu.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kilombero, Mhe. Regina Futakamba alisema kuwa elimu itatolewa kwenye shule za Msingi na Sekondari, Vyuo vya Elimu ya Kati, Sokoni na Stendi ya Mabasi Ifakala.

Upande wa Mahakama KILOSA, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya hiyo, Mhe. Agnes Ringo alisema kwa mwaka 2025 watatoa elimu kuendana na kauli mbiu ya Mahakama, hivyo aliwasihi Wananchi kufika maeneo yaliyowekwa kwa ajili ya kutolea elimu .

Katika Mahakama ya Wilaya ya GAIRO Wiki ya Sheria ilizinduliwa kwa matembezi yaliyofuatiwa na bonanza la michezo mbalimbali. Baadaye Viongozi, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, Bw. Chief Mkama na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Mhe. Irene Lyatuu wakaeleza kuwa wamejiandaa kuwahudumia Wananchi kwa kipindi chote.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Sheria kwa Mahakama Kanda ya Morogoro, kulia kwake ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Latifa Mansoor.

Viongozi, Wadau na Wananchi wengine wakiwa katika  matembezi maalumu ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria.

Wananchi katika Wilaya ya Mvomero  wakiungana katika matembezi maalumu ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mvomero, Mhe. Anthony Ngowi (aliyeshika bahasha) akiwa katika matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria wilayani humo.

Wananchi wilayani Malinyi wakiungana katika matembezi maalumu ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria.

Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mhe. Sebastian Waryuba akizungumza na wananchi (hawapo pichani).

Wananchi wilayani Ulanga wakiungana katika matembezi maalumu ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ulanga, Mhe. Christopher Bwakila akizungumza wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Sheria.

Wananchi wilayani Kilosa wakiungana katika matembezi maalumu ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria.

Wadau wa Mahakama wilayani Kilosa wakiwa katika matembezi hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dustan Kyobya (kushoto) akizungumza na watumishi wa Mahakama na Wadau kabla ya kuanza matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria wilayani humo. Kulia kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kilombero, Mhe. Regina Futakamba.

Wananchi wilayani Kilombero wakiungana katika matembezi maalumu ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Gairo, Mhe. Irene Lyatuu akizungumza na Wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria wilayani humo.

 Shamla shamla za uzinduzi wa Wiki ya Sheria wilayani Gairo zikiendea.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni