Jumanne, 28 Januari 2025

MAHAKAMA KIBAHA YATOA ELIMU KILA KONA WIKI YA SHERIA

Yaanza na wafungwa na mahabusu

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani

Katika kuhakikisha elimu ya sheria inawafikia watu wengi katika kipindi hiki cha Wiki ya Utoaji elimu ya Sheria, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha zikiongozwa na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama hizo, Mhe. Joyce Mkhoi na Mhe. Emmael Lukumai pamoja na wadau wa haki jinai na Haki madai wametoa elimu katika Gereza la Mahabusu Mkuza, lengo kuu likiwa ni kuwafikia wale ambao hawawezi kufika kwenye Vituo vya kutolea elimu vilivyoainishwa.

Wakiwa katika Gereza hilo jana tarehe 27 Januari, 2025, Mahakama na wadau wamepokea changamoto mbalimbali zinazowakabili wafungwa na mahabusu. Mahabusu na wafungwa hao wametoa ushauri wao kuhusu hati za mashtaka, mwenendo wa mashauri na hukumu kuwa katika lugha ya Kiswahili ili waweze kuzielewa kwa kuwa lugha ya Kiingereza inayotumika wengi wao hawaielewi. 

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mhe. Eveline Ntibenda akitoa elimu katika Gereza hilo amewataka wote wenye migogoro wa kikazi wawasilishe maombi yao mapema katika Baraza hilo ili kuepuka kupoteza muda na kupitwa na wakati kisheria, na kusisitiza kwamba, “mara upatapo tu dhamana wahi kufungua shauri lako la mgogoro ili usije tena kuanza na maombi ya kuongezewa muda maana napo lazima uwe na sababu za msingi ndio maombi ya kuongezewa muda yakubaliwe.”

Kwa upande wake Mwakilishi wa Wakala wa Misitu, Bw. Shaban Chaula aliwaeleza Sheria ya Misitu na namna ya kupata vibali halali kama mtu anahitaji kuvuna mazao ya misitu na kusafirisha ili kuepuka kufanya kinyume na sheria. Alieleza zaidi kwamba mazao ya misitu hayaruhusiwi kusafirishwa usiku na hna msako maalum uliofanyika mkoani Pwani wa kukamata wale wote wanaovuna mkaa bila vibali na kusafirisha usiku.

Naye Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bi. Anitha amewataka wafungwa na mahabusu hao wanapokutana na vitendo vya rushwa watoe taarifa kwa kupiga simu ya Bure ambapo amewahakikishia kuwa watoa taarifa huwa wanahifadhiwa na kuna usiri mkubwa baina ya mtoa taarifa na mhusika wa tukio hivyo amewataka wasiwe na hofu katika kutoa taarifa kwa Taasisi hiyo.

Kadhalika elimu ya Mahakama na Sheria kwa ujumla imetolewa pia Shule ya Sekondari Bundikani na katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha. 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani,  Mhe. Joyce Mkhoi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wadau wa Mahakama. Wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai, wa kwanza kushoto ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi, (ASP) Hawa Hamis Juma, wa pili kulia ni Kaimu Mkuu wa Gereza,  Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Eliatosha Yamakili na  wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Mkoa wa Pwani, Mhe. Eveline Ntibenda.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha,  Mhe. Joyce Mkhoi akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Gereza la Mahabusu Mkuza kwa ajili ya kutoa elimu.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni