Jumanne, 28 Januari 2025

UZINDUZI WA WIKI YA SHERIA MWANZA WAFANYIKA


 

Na REHEMA  AWERT-Mahakama, Mwanza 

 

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza,  imefungua Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa kuanza na matembezi yaliyoongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Balandya Elikana aliyemwakilisha  Mkuu wa Mkoa wa Mwanza  akiambatana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza , Mhe. Dkt Ntemi Kilekamajenga.

 

Matembezi hayo yalianzia katika Viwanja vya Furahisha vilivyopo katika jiji la  Mwanza  na kuishia katika Viwanja vya Nyamagana   ambapo watumishi  na wadau mbalimbali wa Mahakama  walipata fursa ya kusikiliza hotuba kutoka kwa viongozi hao.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Elikana aliwahimiza wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuitumia vyema fursa hiyo ya uwepo wa Wiki ya Sheria ambapo watumishi wa Mahakama pamoja na wadau mbalimbali watakuwa wakitoa elimu ya sheria bure kwenye maeneo mbalimbali.


Baadhi ya maeneo hayo ni shuleni, vyuoni, maeneo yenye mkusanyiko wa watu na kutumia vipindi vya redio mbalimbali.

 

Pia aliipongeza Mahakama kwa kuichagua kauli mbiu na kusema  imekuja wakati muafaka ikizingatiwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekea ukingoni mwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na kuanza zoezi la uandaaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050. Sote tunafahamu ya kwamba mchakato huu wa uandaaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo hupitia hatua mbalimbali zinazohusisha wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo. Ikiwemo utoaji na upokeaji wa maoni kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali, zikiwemo taasisi zinazosimamia haki madai nchini.

 

Naye Jaji Mfawidhi alieleza kuwa Mahakama kwa mwaka 2025 imejikita katika kuitafakari haki na ndiyo maana kauli mbiu ya maadhimisho  haya imekuwa na mwelekeo wa kutafakari haki madai katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ifikapo mwaka 2050.

Mhe. Dkt . Kilekamajenga alisisitiza kuwa msingi wa maendeleo na ustawi wa jamii ni amani, na hakuna amani pasipo haki.



 

Jaji Mfawidhi  huyo aliwashukuru wadau wa Mahakama ambao wanashiriki katika utoaji wa elimu kwenye maadhimisho hayo na pia amewakaribisha wananchi kushiriki Siku ya Sheria nchini ambayo itafanyika Februari 3, 2025 katika Viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki(IJC),Mwanza kilichopo maeneo ya Buswelu. 

 

Katika ufunguzi huo, viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali ya Mkoa wa Mwanzawalipata nafasi ya kutembelea mabanda yaliyoandaliwa na kujionea namna Mahakama na wadau walivyojipanga vyema katika zoezi la utoaji elimu kwa wiki nzima

 

(Picha mbalimbali za maadhimisho hayo).

 





(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni