Jumanne, 28 Januari 2025

MAJAJI WA MAHAKAMA YA RUFANI WAFURAHISHWA NA MAADHIMISHO YA WIKI YA SHERIA

Na Magreth Kinabo- Mahakama, Dodoma

 

Majaji wawili wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 28, Januari wametembelea mabanda mbalimbali ya Maadhimisho wa Wiki ya Sheria yanayoendelea katika Viwanja vya Nyerere Square vilivyopo jijini Dodoma na kuupongeza Uongozi wa Mahakamaya Tanzania kwa maandalizi mazuri, ikiwemo kuridhishwa na maelezo ya washiriki wa maonesho hayo.

 

Hayo yalisemwa na Majaji hao, ambao ni Mhe. Augustine Mwarija na Mhe. Lugano Mwandambo wakati wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea  mabanda yaliyopo kwenye viwanja hivyo.

 

“Tunashukuru tumepata maelezo ya shughuli mbalimbali zinazofanyika kutoka kwa wadau walioshiriki kwenye maadhimisho haya, tunaamini kuwa hata wananchi wananufaika na elimu ya kisheria inayotolewa, hivyo tunaushukuru uongozi wa Mahakama kwa maandalizi mazuri na ushirikiano ulioneshwa na wadau wa Mahakama kwani huu ni uhusiano mzuri,” amesema Jaji Mwarija.

 

Jaji Mwarija ameongeza kwamba maadhisho hayo yawe ni endelevu na kushauri kuwa wadau wengine wajiunge ili waweze kutoa elimu ya masuala ya sheria ka ushirikiano.

 

Kwa upande wake Jaji Mwandambo amesema yeye ni mara ya kwanza kutembelea maadhimisho hayo, hivyo amefurahishwa na namna ya washiriki wanavyotoa maelezo kuhusiana na shughuli mbalimbali wanazozifanya wakiwa wachangamfu.

 

Majaji hao, wametembelea banda ya Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), ambapo Mratibu wa RITA Mkoa wa Dodoma, Bw.Mwinyijuma Mushi amewaelezea njisi namna wanavyotoa elimu kuhusu wosia na namna unavyotunzwa na wakati gani unatumika, ikiwemo kupokea maombi 30 ya vyeti vya kuzaliwa tangu maadhimisho hayo yalipoaanza.

 

Banda lingine ni la Jeshi la Zimamoto na Ukoaji, ambapo mshiriki wa maadhimisho hayo, Sajenti Josephat Mlazi ametoa maelezo kuhusu mashine zinazotumika kufungua mlango, bawaba madirisha ya nondo zinavyotumika wakati majanga kama vile moto na ajali.Pia matumizi mazuri ya gesi ya kupikia.

 

Hata hivyo Majaji hao, walitaka kupata ushauri kuwa matumizi mazuri ya kuweka mtungi wa gesi ndani nan je yapi ni sahihi, alijibu kuwa ni vizuri mtungi wa gesi ukajengwa nje ya jiko ili kuepusha majanga ya moto, ikiwemo namna ya kujenga nyumba yenye magirili. 

 

Hivyo Sanjeti huyo aliwataka Watanzania kuwa na tabia kuweka mitungi nje ya jiko ikiwemo kuwasilisha ramani ya ujenzi wa nyumba kwao ili waweze kushauriwa namna ya kujenga madirisha ya nondo kwa ajili ya kuepusha majanga.

 

Katika Banda la Jeshi la Magereza walipata maelezo kuhusu namna wanavyowapokea wafungwa, kuwahifadhi na kuwasindikiza, kutoka kwa Inspekta Vedastus Masasi wa Makao Makuu Dodoma,ambaye aliipongeza Mahakama kutokana na matumizi ya Mahakama Mtandao ambayo imewasaidia kugunguza gharama, kesi kusikilizwa kwa wakati na usalama.

 

“Tunaelimisha wafungwa kufanya shughuli mbalimbali ili waweze kuwa na taaluma, ikiwemo kuwarekebisha tabia. Hapo tuna vifaa ambavyo vimetengenezwa na wafungwa kutoka Gereza la Isanga, Dodoma. Vifaa hivi ni sabuni,vifaa vya urembo, pochi na viatu,” amesema  Inspekta Masasi.

 

Kwa upande wake Jaji Mwarija aliwapongeza jeshi hilo kwa kuzingatia muda wa kufika mahakamani na kazi nzuri wanavyifanya.

 

Mabanda mengine yaliyotembelewa ni TAWJA, BRELA, Benki ya NMB, Idara ya Huduma za Uangalizi na la Chama cha Mawakili wa Serikali.


Sajenti Josephat Mlazi kutoka la Jeshi la Zimamoto na Ukoaji akitoa maelezo kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija(katikati) na Mhe. Lugano Mwandambo(kulia).

Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu, Philbert Kawemama kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi /akitoa maelezo kwa Majaji hao.


 (Picha na Jeremia Lubango- Mahakama)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni