Na CHARLES NGUSA, Mahakama-Geita
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, tarehe 25 Januari,2025 imezindua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kama ilivyo kwa Mahakama nchi nzima.
Maonesho hayo yalizinduliwa katika Viwanja vya EPZA ambapo wananchi na wadau mbalimbali ikiwemo Jeshi la Polisi,Magereza, Zimamoto, Ofisi ya Taifa ya Mashitaka Mkoa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)pamoja na Mawakili wa Kujitegemea walishiriki maandamano hayo ya wiki hiyo.
Uzinduzi huo ulitanguliwa na maandamano ambayo yalianzia katika Viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, yakiongozwa na Mkuu wa Mkao wa Geita, Mhe. Martin Shigela sambamba naye Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe.Kevin David Mhina yaliyohitimishwa katika viwanja vya EPZA.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Geita, Mhe. Martin Shigela akizungumza wakati wa uzinduzi huo,amewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo ya kupata elimu bure kuhusu masuala mbalimbali yanayotolewa katika maonesho hayo.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema “Niwaaase wananchi wote mtumie vyema nafasi hii kuja kupata elimu kwa kuwa wadau wote wanaohusika na haki jinai na haki madai wapo hapa ili kuweza kuongeza uelewa wenu wa mambo ya kimahakama kwa ujumla.”
Kwa upande mwingine Mkuu wa Mkoa amepongeza kasi ya umalizaji wa mashauri katika Kanda hiyo kwa kuwa sasa mashauri yanamalizika ndani ya muda mfupi uliopangwa na pengine hata chini ya muda uliopangwa.
“Nakupongeza Mhe. Jaji Mfawidhi kwa kazi nzuri mnayofanya maana kwa sasa malalamiko yamepungua sana,mashauri yanamalizika ndani ya muda ulipangwa na pengine chini ya muda uliopangwa mfano shauri lililopangwa kumalizika ndani ya mwaka mmoja linamalizika ndani ya miezi sita, lililopangwa kumalizika ndani ya miezi sita linamalizika ndani ya miezi mitatu na lililopangwa kumalizika ndani ya siku mbili linamalizika ndani ya siku moja, haya ni mafanikio makubwa mno ndani ya mkoa wetu,”alisitiza Mkuu wa Mkoa.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe Kevin David Mhina akizungumza wakati wa kumkaribisha Mkuu wa Mkoa alieleza shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika Wiki ya Sheria kuwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa watendaji wa kata katika Halmashauri ya Mji Geita na Halmashuri ya Wilaya Geita kuhusu masuala yahusuyo migogoro ya ardhi, elimu mashuleni,kufanya matendo ya huruma kwa wenye uhitaji pamoja na Mdahalo utakaohusu kutimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Geita.
“Kama mnavofahamu, Mahakama Kuu Kanda ya Geita imetimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake, hivyo tunatarajia kuwa na mdahalo tarehe 29 Januari,2025 juu ya kuanzishwa kwa Mahakama Kuu katika Kanda yetu tujue mafanikio, changamoto na nini kifanyike,” alisema Jaji Mhina.
Washiriki wa matembezi wakiwa barabarani huku wakiwa wamebeba mabango kuelekea katika viwanja vya maonesho.


(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo – Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni