• Afurahishwa na muitikio wa Wadau Wiki ya Sheria
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani leo tarehe 28 Januari, 2025 ametembelea mabanda ya Wadau mbalimbali yaliyopo katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kufanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kutembelea mabanda hayo, Mhe. Dkt. Siyani amekiri kufurahishwa na muitikio mkubwa wa Wadau katika Maonesho ya mwaka huu.
“Nimeguswa na muitikio wa wananchi na Wadau mbalimbali katika Maonesho haya ya Wiki ya Sheria, na nimeona ongezeko la Taasisi mbalimbali mpya katika maonesho hii ni faida hata kwa wananchi kwa kuwa wanapata elimu,” amesema Jaji Kiongozi.
Mhe. Dkt. Siyani amesema kuwa, kadri Taasisi zinavyoshiriki katika Maonesho hayo inawapa fursa wananchi ya kupata elimu kuhusu haki zao na masuala mbalimbali.
Aidha, akizungumzia kuhusu huduma zinazotolewa na baadhi ya wadau walioshiriki katika Maonesho hayo, Jaji Kiongozi ameushauri Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kusogeza huduma za afya/matibabu hadi kwa wananchi waliopo vijijini.
“Tunapotazama Dira ya 2050 hatuwezi kuwa na maendeleo kama wananchi hawana uhakika wa tiba/ matibabu, hivyo nimetoa rai kwa wenzetu wa NHIF kusogeza utoaji huduma za afya hadi kwa wananchi waliopo vijijini, kwakuwa ni vema kila Mtanzania apate fursa ya kutibiwa ili kuwa na afya njema ya kufanya kazi,” ameeleza Mhe. Dkt. Siyani.
Akizungumzia kuhusu kaulimbiu ya Wiki ya Sheria, Jaji Kiongozi amesema eneo la Haki Madai ni muhimu sana kwakuwa linawaleta pamoja Wadau wa Haki Madai ili kwa pamoja waweze kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo.
“Eneo la haki madai linahusu wananchi moja kwa moja, mchakato wa Haki madai unakuwa rahisi sana pale ambapo Sayansi na Teknolojia inatumika na wadau wote,” ameeleza Mhe. Dkt. Siyani.
Jaji Kiongozi ametoa wito kwa Watanzania kutembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria ambayo yanaendelea kufanyika nchi nzima ili waweze kupata elimu kuhusu taratibu za Mahakama na sheria kwa ujumla sambamba na kufahamu haki zao.
“Wiki hii ya Sheria ilianzishwa makusudi ili Mahakama ya Tanzania na Wadau waweze kuwafikia wananchi, hivyo rai yangu kwa wananchi wajitokeze, wapate elimu, waulize, wajifunze ili kujua haki zao na kufahamu masuala mbalimbali,” amesema Mhe. Dkt. Siyani.
Mabanda aliyotemebelea Jaji Kiongozi ni pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Mkemia Mkuu wa Serikali, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na mengine.
Maonesho ya Wiki ya Sheria yanatarajiwa kukamilika tarehe 31 Januari, 2025 huku kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria kikitarajiwa kuwa tarehe 03 Februari, 2025.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni