Jumanne, 28 Januari 2025

RC SHINYANGA ATOA WITO KWA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI WIKI YA SHERIA

. Apongeza Mahakama Kuendeshwa kidigitali

. Amuagiza DC Shinyanga kutangaza kwa siku tatu juu uwepo wa wiki ya elimu ya Sheria Shinyanga

Na EMMANUEL OGUDA, Mahakama-Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha ametoa wito kwa wananchi na Wakazi wa Mkoa huo kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika maeneo mbalimbali inapotolewa elimu ya sheria katika Wiki ya Sheria nchini, 2025.

Mhe. Macha alitoa rai hiyo tarehe 25 Februari, 2025 wakati akizindua maadhimisho ya Wiki ya Sheria mkoani huo ambapo uzinduzi huo ulitanguliwa na matembezi maalum ya zaidi ya kilometa sita (6) yaliyoanzia Viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga na kuhitimishwa katika Viwanja vya Zimamoto, Nguzonane Manispaa ya Shinyanga.

“Elimu ya sheria pamoja na mambo mengine inatolewa hapa, sitegemei baada ya wiki moja mtu anakuja kulalamika hajapata Kitambulisho cha Taifa au mwingine analalamika kuhusu Madalali wa Mahakama ambao leo wapo hapa, wananchi haya yote yanajibiwa katika wiki hii ya sheria kama mnavyoona hapa,’’ alisema Mkuu wa Mkoa huyo.

Aliongeza kuwa, watoa Msaada wa kisheria, Mawakili wa Kujitegemea na hata Taasisi za kifedha pia zipo katika maonesho hayo kuhakikisha kuwa, wananchi wa Shinyanga wanapata elimu ya bure na ya kutosha kuhusu maeneo mbalimbali yanayotolewa huduma kwa wananchi.

Wakati huo huo, Mhe Macha, aliupongeza Mhimili wa Mahakama ya Tanzania kwa kuamua shughuli zake ziendeshwe kidijitali, ambapo alisema, “hakuna tena kutembea na makaratasi, hakuna tena suala la umbali hata kama mtu akiwa hospitali anaweza kuendelea na shughuli za Mahakama kupitia simu yake.’’ 

Aidha, Mhe. Macha alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe Julius Mtatiro kuhakikisha anatangaza kwa wananchi kwa muda wa siku tatu kuhusu uwepo wa maonesho ya utoaji wa elimu kutoka Mahakama na Taasisi mbalimbali zilizopo katika Viwanja vya Zimamoto, Nguzonane pamoja na maeneo mengine ya Mkoa wa Shinyanga.

“Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga nikuombe utafute gari, kuanzia jumatatu, jumanne na jumatano, gari itembee ikitoa maelezo ya shughuli zinazopatikana hapa, gari la matangazo lipite Kata zote za Shinyanga ili wananchi wetu wahudhurie kwa wingi hapa,’’, alisisitiza Mhe Macha.

Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha (katikati) akiongoza matembezi kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Sheria, wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali, Majaji wa Kanda hiyo na sehemu ya Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha akizungumza wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini, 2025 katika Viwanja vya Zimamoto mkoani Shinyanga.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akizungumza wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya wiki ya Shinria nchini katika Kanda hiyo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Gadiel Mariki akifafanua jambo kwa Mgeni Rasmi (hayupo katika picha) wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini, 2025.



Sehemu ya Wadau wa Mahakama Mkoa wa Shinyanga wanaoshiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria, 2025.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)







 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni