Jumamosi, 15 Februari 2025

JAJI JOHN NKWABI KUSIKILIZA MASHAURI NANE YA MAUAJI KIGOMA

Aomba ushirikiano wa wadau kufanikisha usikilizwaji na umalizaji wa mashauri hayo

 Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi amesema kuwa, amejipanga vema kuhakikisha anasikiliza na kumaliza jumla ya mashauri nane ya mauaji yaliyopangwa kusikilizwa katika Kanda hiyo.

Mhe. Nkwabi alieleza hayo tarehe 13 Februari, 2025 wakati wa kikao cha cha kujadili usikilizaji wa mashauri hayo kilichojumuisha Wadau wa Mahakama hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano Mahakama Kuu Kigoma ambapo aliwajuza kwamba kikao cha usikilizaji wa mashauri hayo kitaanza tarehe 17 Februari, 2025.

“Nitahakikisha kuwa mashauri haya yanaisha kama yalivyopangwa, hivyo nawaomba Mawakili wa pande zote kujadili kwa weledi juu changamoto yoyote mnayodhani inaweza kuwa kikwazo katika kuendelea kwa shauri lolote lililopangwa katika kikao hicho,” alisema Jaji Nkwabi.

Aliwataka Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea, upande wa utetezi kama wana changamoto wameombwa kuziwasilisha mapema ili kutatuliwa kabla ya kikao hicho kuanza, hivyo amewasisitiza upande wa upelelezi kuhakikisha wanafikisha wito (summons) kwa mashahidi ili waweze kufika mahakamani kwa wakati na kwa tarehe zilizopangwa.

Sambamba na hayo, Mhe. Nkwabi alisisitiza kuhusu matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) kwenye mashauri ya jinai ili kuepuka kukosea majina ya washtakiwa vilevile shauri kuendelea bila mkwamo unaotokana na makosa ya matumizi bora ya mifumo ya usajili wa mashauri.

“Nawasisitiza kufahamu vema mifumo ya Mahakama na pale mnapokutana na changamoto mtoe taarifa kwa Naibu Msajili haraka ili kutatuliwa mapema,” alisema Jaji huyo.

Naye, Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo alisema kuwa maandalizi ya kikao cha mashauri ya mauaji (Criminal Session) yapo saw ana hakuna changamoto yoyote kwa upande wa Mahakama, hivyo aliwaomba wadau kutoa ushirikiano katika kipindi chote cha kikao hicho ili kuweza kuanza na kumaliza salama kama ratiba ilivyopangwa.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali, Bi. Rehema Mpozemenya alisema kuwa, upande wa Serikali wapo timamu kuhakikisha wanaisaidia Mahakama kutenda haki kwa wakati ili mashauri yaliyopangwa kusikilizwa katika kikao hicho yasikilizwe na kumalizika kama ilivyokusudiwa.

Bi. Rehema alisema kuwa, wito na nyaraka muhimu za mashauri hayo zimeshafika kwa wahusika wa mashauri tayari kufika mahakamani kwa tarehe husika.

Mdau kutoka Magereza, SP. Bosco Lupala alisema kuwa, washtakiwa wapo tayari kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani kwa tarehe husika, hata hivyo alikijulisha kikao kwamba, mshtakiwa mmoja yupo matibabu hivyo wanafanya mawasiliano ili aweze kupata fursa nae ya kusikilizwa na Mahakama kwa tarehe aliyopangiwa katika kikao hicho.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akisisitiza jambo wakati wa kikao cha (pre-session) kilichofanyika tarehe 13 Februari, 2025 katika ukumbi wa Mikutano Mahakama Kuu Kigoma.

Wajumbe wa kikao cha kabla ya usikilizaji wa mashauri (pre-session meeting) wakiwa katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano Mahakama Kuu Kigoma wakijadili mashauri ya mauaji (Criminal Session) yaliyopangwa kusikilizwa katika kikao hicho.

Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo akitoa taarifa ya maandalizi ya kikao cha mashauri ya mauaji (Criminal Session) kwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. John Francis Nkwabi na wadau katika kikao hicho.

Wakili wa upande wa Utetezi, Bw. Eliasadi Msuya akitoa mchango wake katika kikao cha (pre-session) kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano Mahakama Kuu Kigoma.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni