- Jaji Mkuu atoa ushauri mzito kwa Chama
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama,
Dar es Salaam
Rais wa Chama cha
Mawakili wa Serikali, Bw. Amedeus Shayo leo tarehe 14 Februari, 2025 amemtembelea
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa lengo la
kujitambulisha na kufanya naye mazungumzo mafupi.
Bw. Shayo, ambaye ni
Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania, aliwasili ofisini
kwa Jaji Mkuu katika jengo la Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam saa 3.00
asubuhi, akiwa ameambatana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, akiwakilisha Mkoa
wa Dar es Salaam, Bi. Debora Mcharo.
Katika mazungumzo yake, Kiongozi
huyo amemweleza Jaji Mkuu kuwa Mawakili wa Serikali wote ni wanachama wa Chama
anachokiongoza ambacho ni cha kitaaluma na wala hakihusiani na kujihusisha na
harakati za Wafanyakazi.
“Mteja wetu sisi kama
Mawakili wa Serikali ni mmoja, tunasimamia maslahi ya Serikali nchi nzima. Ili
uwe mwanachama lazima uwe Mwanasheria wa Serikali na lazima usajiliwe kwenye
daftari la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, hili ni jukwaa la
kitaaluma, ni vema Mahakama pia ikatutambua,” amesema.
Bw. Shayo amemjulisha Mhe.
Prof. Juma kuwa mwezi wa Aprili 2025 watakuwa na Mkutano Mkuu wa Chama na
wanatarajia, pamoja na wageni wengine, kumwalika Jaji Mkuu ili aweze kushiriki.
Ameahidi ushirikiano na
Mahakama ili Chama hicho kiweze kutoa mchango wake katika shughuli za
kimahakama, ikiwemo Wiki na Siku ya Sheria kwani wanataka kushiriki kikamilifu
kwa upande wao.
Kwa upande wake, Jaji
Mkuu amewapongeza kwa imani kubwa ambayo wamepewa na Mawakili wa Serikali kukiongoza
Chama hicho. Amemweleza Kiongozi huyo kwamba yeye binafsi anakifahamu Chama hicho
kwani amekuwa akihudhuria mara kwa mara kwenye mikutano yao.
Mhe. Prof. Juma amemweleza
Bw. Shayo pia kwamba Chama kina uwezo na wanaweza kutoa mchango mkubwa kwa
Serikali na Mahakama kwa sababu wapo katika kila sehemu ya sheria.
“Ukianza kuangalia wasifu
wa kila mmoja wenu utakuta mpo katika maeneo ya kimaboresho na maendeleo. Lakini
bahati mbaya unaweza kukuta hayo maeneo ambayo mmesomea wengi hamuyatumii,”
Jaji Mkuu amesema.
Ameeleza kuwa Chama hicho
kinaweza kuwa mwamvuli na kuwa na vitengo vya kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali
kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kushauri namna ya kufikia malengo
yanayokusudiwa.
“Rasimu ya Dira ya 2050
imetoa maeneo mengi sana ambayo yanahitaji mabadiliko na maboresho makubwa.
Wakati mwingine ndani yenu mnahitaji kuwa na vitengo vya kufanya utafiti na kutoa
mawazo yenu kwa faragha,” Mhe. Prof. Juma amesema.
Amekishauri Chama hicho
kuanza kuwafahamu wanachama wake na kutambua ujuzi wa kila mmoja ili weweze
kutumia elimu waliyonayo iliyojificha, ambayo hawaitumii, katika maeneo
mbalimbali kama biashara, uwekezaji na masuala ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano.
Viongozi wa Mahakama waliohudhuria ugeni huo ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi na Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Dkt. Jovin Bishanga.
Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Bw. Amedeus Shayo akizungumza alipokutana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo tarehe 14 Februari, 2025.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na mgeni wake (juu na chini).
Viongozi wa Mahakama waliohudhuria ugeni huo. Kutoka kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi na Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Dkt. Jovin Bishanga.
Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Bw. Amedeus Shayo (kushoto) akichukua kumbukumbu muhimu. Kulia ni Wakili wa Serikali Mwandamizi, akiwakilisha Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Debora Mcharo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Bw. Amedeus Shayo (wa pili kulia). Wengine ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (wa pili kushoto), Wakili wa Serikali Mwandamizi, akiwakilisha Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Debora Mcharo (wa kwanza kulia) na Katibu wa Msajili Mkuu, Dkt. Jovin Bishanga
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni