Alhamisi, 13 Februari 2025

MAHAKIMU MTWARA WAPIGWA MSASA MATUMIZI YA MIFUMO

Na HUBERT MAANGA-Mahakama, Mtwara

Mahakama ya Tanzania inazidi kuboresha utendaji kazi kwa watumishi wake kwa kutoa mafunzo kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kisasa ya kielektroniki.

Hivi karibuni, Mahakama Mtwara iliandaa mafunzo maalum kwa Mahakimu wa Mkoa huo, yakilenga kuwajengea uelewa kwenye matumizi ya mifumo kama eJOPRAS, eCMS na DataHub ili kuongeza ufanisi wanapotekeleza majukumu yao.

Mafunzo haya yaliangazia nadharia na vitendo, kuhakikisha Mahakimu wanapata ujuzi wa kina wa matumizi ya mifumo hiyo katika kazi zao za kila siku.

Mfumo wa eJOPRAS ni nyenzo muhimu inayotumika kutathmini utendaji wa Mahakimu kwa haraka na uwazi. Mfumo huo unawawezesha kupokea tathmini kuhusu utendaji wao na kutumia maoni hayo kutoa mrejesho.

Mafunzo hayo yaliwapa Mahakimu uelewa wa kina wa namna ya kutumia mfumo huo kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na mbinu za kuhakikisha tathmini zao zinasaidia kuimarisha huduma kwa Wananchi.

Mfumo huo pia unahamasisha uwajibikaji na uwazi kwa kuwezesha upatikanaji wa taarifa za utendaji kwa urahisi zaidi, jambo linalosaidia Viongozi wa Mahakama kuboresha viwango vya utoaji haki na kuimarisha imani ya Wananchi kwa Mahakama.

Aidha, wakati wa mafunzo hayo, Mfumo wa eCMS ulitambuliwa kuwa nyenzo muhimu katika usimamizi wa mashauri kwa njia ya kielektroniki, kuanzia usajili wa mashauri, kusikiliza na hata kutoa uamuzi.

Mahakimu walipewa mwongozo wa kina kuhusu matumizi ya mfumo huo katika hatua zote za mashauri ili kupunguza ucheleweshaji na kuhakikisha uharaka na uwazi katika utendaji wa Mahakama.

Wakati wa mafunzo pia Mfumo wa DataHub ulielezwa kuwa chombo muhimu unaosaidia kuhifadhi na kufuatilia mashauri, kuhakikisha taarifa zinapatikana kwa urahisi na kwa usahihi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki aliungana na Mahakimu hao katika kuhitimisha mafunzo hayo na kusisitiza kuwa utekelezaji wa mifumo hiyo ni hatua kubwa katika mageuzi ya Mahakama.

Alisema kuwa kwa pamoja, Mahakimu hao wanapaswa kuhakikisha matumizi thabiti ya mifumo hiyo ili kuongeza ufanisi na kuwahudumia Wananchi kwa haraka na kwa haki.

Mhe. Kakolaki aliongeza, "Matumizi ya mifumo ya kielektroniki si tu yanarahisisha kazi za Mahakama, bali pia ni hatua muhimu ya kuondokana na makaratasi yanayosababisha ucheleweshaji na urasimu, ni jukumu letu kukumbatia teknolojia ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa haraka, kwa uwazi na kwa usahihi zaidi."

Mbali na kujifunza kuhusu matumizi ya mifumo hiyo, Mahakimu pia walipatiwa mafunzo kuhusu uendeshaji wa mashauri ya jinai, madai na mirathi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

Walihimizwa kutumia maarifa hayo kwa vitendo ili kuhakikisha mashauri yanasikilizwa kwa wakati, kwa kufuata taratibu za kisheria na kwa usawa kwa wote wanaohusika.

Aidha, Mahakimu hao walishauriwa kushirikiana kwa karibu na Wadau wengine wa mfumo wa haki ili kuimarisha utoaji wa haki kwa Wananchi kwa njia endelevu na yenye uwazi zaidi.

Mratibu wa mafunzo akiwaelezea Mahakimu matumizi ya mfumo wa eJOPRAS.

Mahakimu waliohudhuria mafunzo hayo wakifuatilia kwa umakini, wakiwa na azma ya kupata uelewa wa kina.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (katikati), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe Seraphine Nsana (kushoto) na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mhe. Charles Mnzava katika picha ya pamoja na Mahakimu wanaowakilisha Mahakama zote za Mkoa wa Mtwara mara baada ya mafunzo ya mifumo ya kielektroniki.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni