Na MAGRETH KINABO-Mahakama, Dodoma
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Watendaji wa Mahakama nchini kuwa na umiliki wa bajeti ya Mhimili huo, ikiwemo kuweka mbele vipaumbele vya Taasisi.
Prof. Ole Gabriel ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2024/2025 kwa kipindi cha nusu mwaka na maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kilichoanza leo tarehe 12 Februari, 2025 katika ukumbi wa mikutano kwenye jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania lililopo jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu amesema kuna mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Mahakama ya Utoaji Haki kwa Wote kwa Wakati kutokana na umahiri wa utendaji kazi wa watumishi hao, huku akiwataka kuendeleza ushirikiano katika utendaji kazi.
Akizungumzia kuhusu mapitio ya bajeti hizo, amesema umiliki wa bajeti uko kwa watendaji wa Mahakama mbalimbali nchini. Hivyo wanawajibika katika masuala ya rasilimali watu na majengo.
“Ninyi Watendaji wa Mahakama kila mmoja anatakiwa kuwa na umiliki wa bajeti, pia kuendelea kuwa na nidhamu ya matumizi mazuri ya fedha za umma,” amesema Prof. Gabriel.
Prof. Gabriel akielezea kuhusu Dira hiyo amesema imetafsiriwa vizuri katika Mpango Mkakati wa Mahakama ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (2020/2021- 2024/2025).
"Mpango Mkakati huu ni nyenzo muhimu inayotuongoza katika kupanga na kutekeleza vipaumbele kwa kila mwaka wa fedha ili kufikia malengo tuliyojiwekea katika suala zima la utoaji haki kwa wananchi," amesisitiza.
Ameongeza kuwa, maandalizi ya Bajeti ya kila mwaka ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama. "Hatuna budi kutekeleza suala hili kwa umakini mkubwa, ili kuleta tija na ufanisi, "amesisitiza.
Amewasihi wajumbe hao kubainisha maeneo ya kuboresha katika kipindi kilichosalia, pamoja na mwaka ujao wa fedha (2025/26) ikiwemo kutoa rai kwa kila mmoja kushiriki kikamilifu zoezi hilo, ili kutoa mchango katika kufikia malengo.
Prof. Gabriel amewaasa wajumbe kikao hicho, kuwa wabunifu wa kutatua jambo au changamoto wanazokutana nazo kwa kuwa wao ni viongozi katika maeneo wanayosimamia kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda (MMK-K) na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni (MMK-D).
Katika hatua nyingine Mtendaji Mkuu huyo, amewataka wajumbe wa kikao hicho kutoa michango mbalimbali katika mapitio ya bajeti, ambapo Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, Bw. George Mbara amesema kupitia bajeti ya mwaka huu wa fedha kumekuwa na mafanikio kwani miradi ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo, Wilaya, Mahakama Kuu na IJC inaendelea vizuri.
Amefafanua kuwa miradi inaendelea chini ya usimamizi mzuri hali iliyosabababisha utulivu kwenye maeneo ya kazi.
Bw. Mbara ameongeza kuwa kuna changamoto ambayo ipo kwa baadhi ya wakandarasi ambao hawana uwezo wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa upande Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Amiri Msumi amesema kazi iliyopo kwa sasa katika majengo hayo kupambana kupata fedha kwa ajili ya kuongeza gharama za uendeshaji kwa kuzingatia bajeti halisi za gharama za urekebishaji.
Pia Mhe. Msumi amesema vikao vya kesi za mauaji gharama zake zimepanda kutokana na kuwepo kwa Wakili zaidi ya mmoja au mashahidi, hivyo gharama hizo zinatakiwa kuangaliwa uhalisia wake.
Awali akizungumza wakati wa utangulizi wa kikao hicho cha siku tatu, Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Ufuatiliaji, Bw. Erasmus Uisso amesema, “lengo la kikao hiki ni mapitio ya bajeti, ambapo tunatamani yawe shirikishi, na wajumbe wanatakiwa kushiriki katika hatua za awali. Kazi hii inafanyika katika kipindi cha siku tatu, hivyo tuko katika hatua mwisho."
Kikao hicho kimejumuisha Watendaji wa Mahakama-Kanda na Mikoa, Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu na Masjala, Mahakimu Wakazi Wafawidhi, Maafisa Bajeti, wachambuzi wa bajeti na baadhi ya Viongozi kutoka Makao Makuu.
Picha za chini ni sehemu ya washiriki mbalimbali wa kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni