Jumatano, 12 Februari 2025

SIMAMIENI VEMA MIKAKATI YA TAASISI; MSAJILI MKUU

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya ametoa rai kwa Watendaji, Wasajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi pamoja na Maafisa Bajeti wa Mahakama nchini kusimamia vema mikakati ya Taasisi ili huduma ya utoaji haki iweze kupatikana kwa wananchi kwa wakati.

Mhe. Nkya ametoa rai hiyo leo tarehe 12 Februari, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Mapitio ya Bajeti ya 2024/2025 na Maandalizi ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.

“Kwa mwaka jana kwenye ngazi zote za Mahakama tulifanya vizuri sana katika eneo la usikilizaji wa mashauri na baadhi ya Mahakama zilimaliza mwaka bila mlundikano wa mashauri, hivyo nitoe rai kwenu kuendelea kusimamia mikakati tuliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kupanga vizuri vikao vya Mahakama,” amesema Msajili Mkuu.

Amesema kwamba, ni muhimu kuratibu na kusimamia vema utekelezaji wa bajeti kwa kuhakikisha kuwa inakuwa shirikishi sambamba na kuzingatia vipaumbele vya Mahakama ambavyo mojawapo ni usikilizaji wa mashauri.

Amewakumbusha pia kuendelea kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika mchakato mzima wa usikilizaji wa mashauri ambapo ameeleza kuwa kwa sasa ngazi zote za Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Rufani zinatumia mfumo wa Kieletroniki wa Usajili na Usimamizi wa Mashauri (CMS).

Kadhalika, Mhe. Nkya amedokeza kuhusu umuhimu wa Viongozi hao kuendelea kufanya kaguzi za Mahakama pamoja na kusimamia nidhamu na maadili ya watumishi ili kuendelea kujenga imani ya wananchi kwa Mhimili huo.

Akizungumza katika kikao hicho cha siku tatu, naye Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kufanya mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya Mahakama ya mwaka wa fedha 2024/2025 kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia Julai-Desemba, 2024 sambamba na uchambuzi wa maoteo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.



Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akizungumza wakati wa Kikao cha Mapitio ya Bajeti ya 2024/2025 na Maandalizi ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kilichoanza leo tarehe 12 Februari, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Meza kuu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) wakiwa katika kikao cha Mapitio ya Bajeti ya 2024/2025 na Maandalizi ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026. Wa pili kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, wa pili kulia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda, Bw. Leonard Magacha na wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu-Divisheni, Bi. Mary Shirima.


Picha mbalimbali za washiriki waliohudhuria katika kikao cha Mapitio ya Bajeti ya 2024/2025 na Maandalizi ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 leo tarehe 12 Februari, 2025.
 
Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso akizungumza jambo wakati wa kikao cha Mapitio ya Bajeti ya 2024/2025 na Maandalizi ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 leo tarehe 12 Februari, 2025.

 
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tazania-Kanda, Bw. Leonard Magacha akizungumza jambo wakati wa kikao cha Mapitio ya Bajeti ya 2024/2025 na Maandalizi ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 leo tarehe 12 Februari, 2025.  Kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya.
 



Picha mbalimbali za makundi kati ya meza kuu na Washiriki wa Kikao  cha Mapitio ya Bajeti ya 2024/2025 na Maandalizi ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 

Picha ya pamoja, katikati ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, wa tatu kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, wa tatu kulia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu- Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick, wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tazania-Kanda, Bw. Leonard Magacha, wa pili kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu-Divisheni, Bi. Mary Shirima na wa pili kulia ni Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sundi Fimbo.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)













Hakuna maoni:

Chapisha Maoni