- Asisitiza watumishi kujiendeleza kitaaluma
Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim amesisitiza watumishi kujiendeleza katika taaluma mbalimbali ili waweze kwenda na mabadiliko na kasi ya matumizi makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mahakamani.
Mhe. Ebrahim alitoa wito huo wakati wa kikao cha menejimenti Kanda ya Morogoro kilichofanyika jana tarehe 10 Februari, 2025 kwenye Ukumbi wa Mikutano katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.
Alisisitiza kuwa kwa sasa Mahakama imejikita zaidi kwenye matumizi ya TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu yake, hivyo ni jambo la msingi kwa watumishi kuwa na taaluma zaidi ya moja ili kuleta tija kazini.
Alitoa mfano wa Majaji na Mahakimu ambao kwa sasa wanasikiliza mashauri kwa njia ya mtandao na kufafanua kuwa ingewawia vigumu wao kutekeleza majukumu yao kama wasingekuwa na uelewa wa matumizi ya vifaa vya TEHAMA, ikiwemo kompyuta na mifumo iliyoanzishwa na Mahakama.
“Lakini kwa kuona umuhimu huo Mahakama ya Tanzania imekuwa ikiwapatia mafunzo ya mara kwa mara. Ni vyema tuhamasishane sisi wenyewe na watumishi wenzetu wajiendeleze kwenye fani mbalimbali kwa kuwa Mahakama ya sasa sio ya zamani…
“…Tusikubali mabadiliko haya yakatuacha, kama mtu ana fani ya udereva pamoja na teknolojia anaweza pia kutumika kwenye shughuli za TEHAMA mara anapokuwa ameshamaliza majukumu yake ya udereva,” alisema.
Sanjari na hilo, Jaji Mfawidhi alitoa rai kwa Viongozi wa Mahakama Kanda ya Morogoro kuwasikiliza watumishi wote bila kubagua kwani anatamani kuona kazi inafanyika kwa upendo na ushirikiano.
“Utamaduni wangu napendezwa sana tukienda kwa pamoja na tukafanikisha jambo kwa pamoja na sio kuwatanguliza baadhi ya watu mbele, halafu wengine tukabakia nyuma, hatutafika. Viongozi wapeni nafasi watumishi ya kuwafikia na kuwashirikisha masuala yanayowakabili, twendeni tukafanye kazi kwa upendo na tuhurumiane, hapo ndipo tutakapofikia lengo” alisema.
Kikao hicho kilihudhuliwa pia na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro akiwemo Mhe. Stephen Magoiga na Mhe. Aisha Sinda, Mtendaji wa Mahakama, Bw. Ahmed Ng’eni, Naibu Msajili, Mhe. Susan Kihawa, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Janeth Kinyage, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya zote, Maafisa Utumishi pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo.
Sambamba na hilo, kikao hicho pia kilipokea taarifa ya mashauri ya kanda nzima pamoja na taarifa ya kiutawala na baadaye kupeana mikakati ya utekelezaji wa majukumu ndani ya mwaka 2025.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni