· Awataka kutenda Haki na Kutunza Siri
Na Lydia Churi- Tume
ya Tumishi wa Mahakama, Songea
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea
Mhe. James Karayemaha amewaapisha baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maadili ya
Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na ngazi ya Wilaya na kuwataka wajumbe hao kutekeleza
majukumu yao kwa kutenda haki.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha wajumbe hao jana
mjini Songea, Jaji Mfawidhi pia aliwataka wajumbe wote wa Kamati za Maadili ya
Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na Wilaya kutekeleza jukumu lao la msingi la
kusimamia maadili ya Mahakimu kwa uaminifu na kwa weledi.
”Tendeni haki mnapotekeleza jukumu lenu la msingi la
usimamizi wa maadili na nidhamu ya Mahakimu, muwe na utamaduni wa kutoa nafasi
ya kuwasikiliza wale wanaofikishwa mbele ya Kamati zenu ili muweze kutenda
haki”, alisema Mhe. Karayemaha.
Wajumbe walioapishwa ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Bw.
Kapenjama Ndile ambaye anakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa
Mahakama wilaya ya Songea na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Songea Mhe. Asha Hassan Waziri ambaye anakuwa ni Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya
Mkoa wa Ruvuma. Aidha, Mwalimu Mstaafu mama Ngwala pia aliapishwa kuwa Mjumbe
wa Kamati hiyo.
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za
Maadili yanayoratibiwa na Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, Jaji
Karayemaha alisema yana umuhimu mkubwa kwa kuwa yatawajengea uwezo na
kuwaimarisha wajumbe katika utekelezaji wa majukumu yao.
Jaji huyo aliwakumbuka wajumbe umuhimu wa kutunza siri za
kamati na kufanya uamuzi wa pamoja wanapokuwa katika vikao vya kamati.
Aliongeza kuwa wajumbe hao hawana budi kuwa kioo cha wengine kwa kuwa na
maadili na nidhamu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Mwenyekiti wa Kamati ya
Maadili ya Maafisa Mahakama mkoani humo Col. Ahmed Abbas Ahmed amewasisitiza wajumbe wa Kamati ya Mkoa kukutana na
kufanya vikao vya kamati na kuhakikisha vikao hivyo vinafanyika kwa wakati kwa
mujibu wa Sheria.
Aidha aliwataka wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa
Mahakama ngazi ya Mkoa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia maadili na nidhamu
ya Mahakimu kwa kufuata taratibu na Sheria zilizowekwa.
Kuhusu kuwezesha kufanyika kwa vikao vya Kamati, Mkuu
huyo wa Mkoa aliagiza kutengwa kwa bajeti ya kuwezesha vikao hivyo.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo
cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya
Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili
kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la
kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja
na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa
Mahakama Sura ya 237.
Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya
watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia
kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura
ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye Kamati
zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya
Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea Mhe.
James Karayemaha akimuapisha Mkuu wa Wilaya ya Songea Bw. Kapenjama Ndile kuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya Wilaya ya Songea jana
mkoani Ruvuma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea Mhe.
James Karayemaha akizungumza
Sehemu ya Wajumbe Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya
Mkoa na Wilaya wakiwa kwenye Mafunzo kuhusu uendeshaji wa Kamati hizo jana
mkoani Ruvuma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea Mhe.
James Karayemaha (katikati) akiwa katika mafunzo na hafla ya kuwaapisha wajumbe
wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na Wilaya jana mjini
Songea. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Col. Ahmed Abbas Ahmed na kulia ni
Naibu Katibu (Maadili na Nidhamu) wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Col. Ahmed Abbas Ahmed (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na Wilaya mara baada ya kumalizika kwa Mafunzo kuhusu Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama jana mkoani Ruvuma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni