Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imefanya hafla fupi ya kumpokea Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Frank Mirindo aliyehamishiwa katika Kanda hiyo sambamba na kumuaga aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe.Dkt. Mwajuma Kadilu ambaye amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Hafla hiyo ilifanyika jana tarehe 10 Februari, 2025 katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na kuhudhuriwa na Majaji, viongozi na watumishi wa Kanda hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Dkt. Kadilu aliwashukuru watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwa ushirikiano na upendo mkubwa waliompatia wakati wote wa utumishi wake akiwa katika Kanda hiyo na kuongeza kwamba alikuwa na furaha ya kufanya kazi na timu imara na yenye ufanisi hali ambayo ilimuwezesha kutekeleza majukumu yake bila kikwazo chochote.
“Nimefurahi sana kufanya kazi na timu hii ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, ushirikiano wenu na upendo mkubwa mliyonionyesha umenisaidia kutekeleza majukumu yangu bila kikwazo chochote, na kwahiyo nawashukuru sana,” alisema Jaji, Mhe. Dkt. Kadilu.
Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Frank Mirindo naye alieleza furaha yake ya kuanza kazi katika Kanda hiyo kongwe, ambayo ina historia ya mashauri mengi makubwa na yenye mvuto katika tasnia ya sheria nchini.
"Kanda hii imekuwa na mchango muhimu katika maamuzi ya kimahakama na miongozo ya kisheria ambayo imekuwa ikitumika kama rejea na msingi wa kufanya maamuzi mengi ya kisheria hadi sasa," alisema Mhe. Dkt. Mirindo.
Viongozi wa Mahakama pamoja na watumishi walimpongeza Jaji Kadilu kwa usikivu, kujituma na mchango wake mkubwa katika kuboresha mfumo wa haki na walimtakia mafanikio katika Kanda ya Dar es Salaam alipohamishiwa.
Aidha, watumishi hao pia wamemkaribisha Mhe. Dkt. Mirindo katika Kituo hicho na kumtakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yake.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi (aliyesimama) akizungumza jambo jana tarehe 10 Februari, 2025 wakati wa hafla ya kumuaga aliyekuwa Jaji wa Kanda hiyo, Mhe. Dkt. Mwajuma Kadilu na kumpokea Jaji, Mhe.Dkt. Frank Mirindo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Zainabu Mango, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Mwajuma Kadilu na wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Frank Mirindo.





.jpg)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni