Jumatatu, 10 Februari 2025

MAJAJI WA MAHAKAMA YA RUFANI TANZANIA WAANZA VIKAO VYA KUSIKILIZA MASHAURI DODOMA

Na MAGRETH KINABO-Mahakama, Dodoma

 

Jumla ya Majaji sita wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 10 Februari, 2025 wameanza  vikao vya kusikiliza mashauri  52 mbalimbali  ya madai  katika majopo ya makundi mawili kwenye jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania lililopo jijini Dodoma.

 

Kwa mujibu wa Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Omari Kingwele aliwataja Majaji waliopo katika jopo la kundi A kuwa ni Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira.Majaji wengine ni Mhe.Zepharine Nyalugenda Galeba na Mhe.  Mustapha   Kambona   Ismail.

 

Naibu Msajili huyo amesema Majaji hao wanatarajia kusikiliza mashauri 26, ambayo ni  ya mlundikano yanayohusu masuala ya kodi na biashara.

 

Katika hatua nyingine Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Charles Magesa amesema jopo lingine la kundi B la Majaji watatu, ambao ni Mhe. Rehema Kerefu, Mhe. Patricia Saleh Fikirini na Mhe. Benhajj Shabaan Masoud litasikiliza mashauri 26, ambayo ni kodi, biashara na ardhi.

 

Majaji hao wanatarajia kumaliza vikao hivyo vya kusikiliza mashauri hayo tarehe 28 Februari, 2025.

 

Baadhi ya Majaji  sita wa Mahakama ya Rufani Tanzania waliowasili jijini Dodoma kwa ajili kuanza vikao vya kusikiliza mashauri ya  madai katika  jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania lililopo jijini Dodoma. wakiwemo wawili wapya walioripoti kwenye kituo chao cha  kwanza cha kazi wakiwa katika pichaya pamoja.


Baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania waliowasili jijini Dodoma kwa ajili kuanza vikao vya kusikiliza mashauri wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania wakiingia katika ukumbi namba moja  kwa ajili ya  kuanza vikao vya kusikiliza  mashauri. 

Baadhi ya Mawakili wakijiandaa kwa ajili ya vikao vya mashauri hayo.

 

  


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni