Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi leo tarehe 26 Februari, 2025 amefungua
mafunzo yanayohusu Kanuni za Maadili ya Kimahakama (Bangalore Principles) kwa
Mahakimu Wakazi 30 wa Mahakama za Wilaya kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanafanyika katika Hoteli
ya Four Points by Sheraton jijini Dar es Salaam. Yameandaliwa na Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), kwa ufadhili wa Shirika la Ushirikiano wa
Kimataifa la Ujerumaini (GIZ), kupitia mradi wake wa Ukuzaji wa Utawala wa
Sheria na Mahakama Barani Afrika (Promotion of Rule of Law and Judiciary in
Africa-ProLA).
Wawezeshaji wa mafunzo
hayo ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim
Tiganga na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Lilian
Itemba.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Maghimbi amewahimiza watumishi wa Mahakama kuzingatia maadili na kuendelea kuwajibika kwa umma wakati wa kutekeleza majukumu ya utoaji haki.
Jaji Maghimbi amewaambia washiriki kwamba kanuni za Bangalore hutoa mfumo
wa jumla unaosaidia Majaji na Mahakimu kukabiliana na changamoto za kimaadili
kwa namna ambayo inahakikisha uhuru, kutopendelea na uwajibikaji.
“Kanuni hizi za uhuru wa kimahakama ni nguzo muhimu kwenye wajibu wetu
kwani zinatuongoza kwenye matendo yetu ndani na nje ya Mahakama na kutusaidia
kudumisha imani ya umma tunaohudumia,” amesema.
Jaji Maghimbi amebainisha kuwa katika ulimwengu wa kisasa unaoendelea kwa
kasi, Majaji na Mahakimu wanakabiliwa na matatizo yanayoongezeka ya kimaadili,
kuongezeka kwa mitandao ya kijamii na utata wa masuala ya kisasa ya kisheria, ambayo
yote yanawahitaji kuwa makini zaidi kimaadili.
Kwa hivyo, amewaeleza washiriki kuwa mafunzo kama hayo yatawawezesha
kubaini changamoto kama hizo na kubadilishana maarifa juu ya jinsi wanavyoweza
kutumia kanuni za Bangalore kwa ufanisi katika mamlaka zao.
Jaji Maghimbi aliwakumbusha washiriki hao pia kuwa katika muda wa siku tatu
za mafunzo hayo, wawezeshaji watawaelekeza jinsi maadili yao yanavyochangia kwenye
kufanya maamuzi na nini wafanye ili kuhakikisha wanaendana na majukumu yao ya
kikazi.
Naye Mshauri wa Kisheria GIZ Tanzania, Bi Neema Ndemno aliwaambia washiriki
wa mafunzo hayo kuwa kama Maofisa wa Mahakama wana wajibu wa kipekee na muhimu
wa kusimamia sheria na kulinda haki za watu wote wanaofika mbele yao.
Alieleza kuwa mienendo ya Maofisa wa Mahakama, kitaaluma na kibinafsi, ina
mchango mkubwa katika kudumisha uadilifu na kuhakikisha haki inatolewa kwa haki
na bila upendeleo.
Malengo ya mafunzo
hayo ni kuwajengea uwezo washiriki hao juu ya ufahamu wa kanuni hizo ili
waendelee kutenda kazi zao za utoaji wa hukumu kwa uhuru, uadilifu, umahiri na
bila upendeleo.
Kanuni za Bangalore ziliundwa mwaka 2002 na jopo la Majaji Wakuu na Majaji Waandamizi kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa (UN) na zinatoa muongozo wa kanuni za maadili ya Kimahakama ili kuhakikisha taaluma hiyo inazingatia misingi ya uadilifu, uhuru, usawa, umahiri na bila upendeleo.
Mahakama ya Tanzania ina kanuni kama hizo za mienendo na maadili za mwaka 2020 kwa ajili ya Maafisa wake ambazo zilitungwa chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011. Kanuni hizi zinawataka maofisa wa Mahakama kuzingatia uadilifu, uhuru, ustaarabu, umahiri, bila upendeleo na usawa.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu nyingine ya Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Wilaya (juu na chini) wanaohudhuria mafunzo hayo.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Sekretariet. Picha chini ni Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni