Na ASHA JUMA - Mahakama Morogoro
Kufuatia maboresho makubwa ya Mahakama katika matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), tarehe 24 Februari, 2025 Watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro walipatiwa mafunzo ya matumizi ya mifumo mbalimbali.
Akizungumza wakati anafungua mafunzo hayo, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga aliwataka Watumishi wote kushiriki kikamilifu kwani yana tija katika majukumu yao ya kazi za kila siku.
“Mafunzo haya yana umuhimu kwetu sote, hivyo ninaagiza kila Kiongozi kwenye eneo lake ndani ya Mahakama kwenye Kanda ya Morogoro ahakikishe Watumishi walio chini yake wanashiriki kikamilifu, lazima wote twende kwa pamoja na maboresho makubwa yanayofanywa na Mahakama,” alisisitiza Mhe. Magoiga.
Aidha, Mhe. Magoiga alitoa rai kwa Watumishi ambao wanaujuzi na masuala yeyote ambayo yatasaidia kufanikisha utendaji kazi kwa ufanisi zaidi wawasilishe mawazo yao kwenye uongozi ambao utayapitia na kujiridhisha ili kuandaa mafunzo ya ndani kwa ajili ya kushirikishana uzoefu.
“Niseme tu kama kuna mtu ana ujuzi wa jambo lolote ambalo litatusaidia kutekeleza majukumu yetu, asisite kuja kutushirikisha nasi tutaandaa mafunzo ya ndani ili wote tupate uelewa wa pamoja, lengo ni kuhakikisha kazi inafanyika kwa ubora,” alieleza Mhe. Magoiga.
Mafunzo hayo yanayotolewa na Wawezeshaji kutoka Kitengo cha TEHAMA ndani ya Kanda ya Morogoro yanategemewa kuhitimishwa kesho tarehe 27 Februari, 2025.
Miongoni mwa mada zitakazotolewa ni pamoja na matumizi na maboresho ya mifumo, matumizi sahihi ya mitandao na usalama wake yanayotumika katika shughuli mbalimbali za kimahakama.
Mafunzo hayo pia yamelenga kuwafikia Watumishi wa ngazi zote ndani ya Kanda ya Morogoro. Watumishi waliopo wilayani wanapokea mafunzo hayo kwa njia ya mtandao.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni