Ijumaa, 28 Februari 2025

MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI PWANI MAMBO SAFI

  • Hakuna mashauri ya Mlundikano
  • Wadau wa Haki Jinai Pwani waweka mikakati zaidi kuthibiti mlundikano

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani

Katika kuhakikisha  kuwa hakuna mlundikano wa mashauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, Mahakama hiyo imefanikiwa kuyaondoa mashauri yote yaliyokuwa yanaashiria mlundikano  licha ya kuwa Mahakama hiyo kubaki na Hakimu mmoja pekee baada ya mwingine kustaafu.

Akizungumza leo tarehe 28 Februari, 2025 katika Kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi amesema mashauri yote ambayo Mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza hayajafikia kuwa mashauri ya muda mrefu kutokana na kwamba yapo ndani ya miezi mitatu isipokuwa shauri moja ambalo limepangwa kusikilizwa kwa mfululizo ili limalizike kwa wakati lisisababishe mlundikano.

Aidha, Mhe. Mkhoi amewapongeza wadau wa haki jinai kwa ushirikiano wao ambapo amesema kuwa, nguvu kubwa na juhudi zimeonekana mpaka hatua   waliyofikia kwa sasa.

Akizungumzia kuhusu mashauri ambayo yanahitaji utafsiri, Mfawidhi huyo amewaomba Polisi kusaidia kwa kuhifadhi mawasiliano ya mtafsiri ambaye ametafsiri wakati mshtakiwa akiwa Polisi aweze kufika pia mahakamani ili kuokoa muda na kumaliza shauri kwa haraka kuliko kuanza upya kutafuta mtafsiri mwingine ambapo kwa Mkoa wa Pwani upatikanaji wao ni mgumu.

Amewaomba pia Polisi kufanya upelelezi kwa haraka kwa mashauri ambayo Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza ili yakamilike na kwenda Mahakama yenye mamlaka ili kuepuka pia msongamano kwa Mahakama yenye mamlaka na kusikiliza shauri hilo.

Katika kikao hicho maazimio mawili yamefikiwa ambayo ni pamoja na ukamilishaji wa upelelezi kwa haraka kwa mashauri ambayo upelelezi wake haujakamilika na kuhakikisha mashahidi wanafika mahakamani kwa wakati ili mashauri yakamilike kwa wakati.

Kikao hicho kilitanguliwa na kutembelea magereza na kuzungumza na Mahabusu katika Gereza la Mahabusu Mkuza ambapo wadau wa haki jinai walisikiliza changamoto mbalimbali na kuweza kuzitafutia ufumbuzi zaidi.

Malalamiko mengi yameelekezwa katika Jeshi la Polisi ambapo mahabusu hao wamelalamika kwamba, wanapokuwa polisi hawapewi haki zao kabla ya kutoa maelezo. Wamemuomba Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha kuzungumza na Polisi ili wazingatie sheria na kuwapa watuhumiwa haki zao kabla ya kuwaandika maelezo yao.

Mahabusu hao wameongeza kuwa maelezo mengi ya onyo yanayotolewa Mahakama hayakutolewa kwa hiari isipokuwa tu ushahidi wa kuthibitisha kutokana na kwamba hakuna shahidi anayeweza kutoa ushahidi kuhusiana na suala la kutopewa haki wakati wa kuchukuliwa maelezo.

Mwenyekiti wa Kikao cha Kusukuma Mashauri ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (kushoto) akiongoza kikao hicho kilichofanyika leo tarehe 28 Februari, 2025 kwenye ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha. Kulia ni Wakili wa Serikali Mwandamizi, Gladness Mchami ambaye ni Katibu wa kikao hicho.

Wajumbe wa Kikao cha Kusukuma Mashauri  wakiendelea na kikao.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi  Kibaha-Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (katikati) na wadau wengine wa Mahakama hiyo wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza kupokea malalamiko/changamoto kutoka kwa Mahabusu wa Gereza la Mkuza. Kushoto kwa Mhe. Mkhoi ni  Kaimu Mkuu wa Gereza la Mkuza, Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Eliatosha  Yamakili, kwa kwanza kulia ni Afisa Adhabu Mbadala (Probation Officer), Bw. Deogratuas Njuu. Wa pili kushoto ni  Kaimu Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Pwani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Khatibu Sanduku na wa kwanza kushoto ni Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Matilda  Zakaria.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni